STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, February 15, 2013

Sikinde yapata mdhamini ikijiandaa kwenda Marekani

Baadhi ya wanamuziki wa Sikinde wakiwajibika

WAKATI safari yao ya kwenda Marekani ikisubiri ujio wa mfadhili wao mwezi ujao, bendi kongwe ya muziki wa dansi nchini, Mlimani Park 'Wana Sikinde' imepata mdhamini kwa ajili ya kurekodi nyimbo zake.
Kwa mujibu wa Katibu wa bendi hiyo, Hamisi Milambo alimtaja mdhamini huyo kuwa ni Werner Grabner, raia wa nchi ya Ujerumani, ambaye atagharamia kazi ya kurekodi baadhi ya nyimbo mpya na za zamani za Sikinde kwa lengo la kuitangaza kimataifa.
Milambo alisema Mjerumani huyo atagharamia kazi ya kurekodi 'audio' na video kwa kile kilichoelezwa na wanasikinde kwamba amevutiwa na ukali wa bendi hiyo aliyokuwa akiifuatilia kwa muda mrefu bila Sikinde kufahamu.
Katibu huyo aliongeza kuwa neema hiyo imewaangukia wakati wakijiandaa kumpokea mfadhili wao mwingine kutoka Marekani kwa ajili ya kumalizia mipango yao ya kwenda nchini humo kutumbuiza na kurekodi.
Milambo alisema mfadhili huyo anatarajiwa kutua mwezi ujao ili kuweka mambo sawa kabla ya Sikinde kupaa kuelekea kwa 'Obama'.
"Safari yetu ya Marekani ipo kama tulivyoitangaza, tulikuwa tunasubiri kumalizana na mfadhili wetu atakayetua nchini mwezi ujao baada ya awali viongozi wenzetu kwenda kufanya mazungumzo ya awali nchini humo," alisema Milambo.
Aidha aliongeza bendi yao imenyakua wanamuziki wapya akiwemo mkongwe, Adolph Mbinga 'Mtuhumiwa' aliyeanza kuonekana kwenye maonyesho yao huku wengine walitarajiwa kutambulishwa katika maonyesho yao ya mwishoni mwa wiki.
Sikinde ilipata pigo kwa kupoteza baadhi ya nyota wake, mmoja akifariki na wengine watatu wakihamia kwa wapinzani wao Msondo Ngoma akiwamo Athuman Kambi.

No comments:

Post a Comment