MAKALLA AIPONDA KAMATI YA MTIGINJOLA
NAIBU Waziri wa Habari, Vijana, Utamduni na Michezo, Amos Makalla, ameiponda Kamati ya Rufani ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa kitendo chake cha kumuengua Jamal Malinzi kuwania urais wa
shirikisho hilo.
Makalla amesema kitendo hicho kimemsikitisha kwa vile sababu zilizotolewa na kamati hiyo kuhusu uamuzi huo hazina msingi na zimeonyesha ubabaishaji mkubwa.
Naibu Waziri huyo amesema sababu hizo zinatia shaka na zimekosa ushawishi, ambao unaweza kueleweka kwa wadau wa soka nchini.
Makalla alisema hayo juzi alipokuwa akihojiwa katika kipindi cha Michezo Extra kilichorushwa hewani na kituo cha redio cha Clouds FM.
Kamati ya Rufani ya TFF chini ya Mwenyekiti wake, Idd Mtiginjola, mwanzoni mwa wiki hii ilimuengua Malinzi kuwania nafasi ya urais katika uchaguzi mkuu wa shirikisho hilo utakaofanyika Februali 24, mwaka huu kwa madai ya kukosa sifa.
Makalla alisema kitendo kilichofanywa na kamati hiyo kimeishushia heshima ikiwa ni pamoja na kutilia shaka maamuzi yao, ambayo ameyaita kuwa ni mepesi.
"Bila kupepesa macho wala kuumauma maneno, nikiwa mdau wa soka na kuuvua wadhifa wangu wa unaibu waziri, hapa kuna tatizo kwani kamati haijamtendea haki Malinzi," alisema Makalla.
Naibu Waziri alisema kamati hiyo haikuwa na hoja za msingi na sababu zilizotolewa zimekosa nguvu na haziwezi kukubalika kwa mtu yeyote mwenye mapenzi ya soka ya Tanzania.
Alisema uamuzi huo unaweza kusababisha kuibuka kwa machafuko na kuirudisha TFF kwenye migogoro iliyodumu kwa miaka mingi miaka ya 1980 hadi 1990. Alisema ipo haja ya uamuzi huo kutazamwa upya.
"Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete amefanya kazi kubwa sana katika kusimamia soka ya Tanzania ili izidi kufanikiwa, sasa baada ya kufanikiwa tusitake kurudisha nyuma maendeleo hayo," alisisitiza Makalla.
Mbali ya Makalla, wadau wengi wa soka nchini wamelalamikia uamuzi wa kamati hiyo kwa madai kuwa, umefanywa bila kuzingatia ukweli wa mambo na kulenga kuwabeba baadhi ya wagombea.
No comments:
Post a Comment