BONDIA mkongwe wa ngumi za kulipwa nchini, Maneno Osward 'Mtambo wa Gongo' anatarajiwa kuvaana na Robert Mrossy 'Cobra' katika pambano la Middleweight, litakalofanyika Machi 20 mwaka huu.
Osward mwenye miaka 41 atapigana na Cobra katika pambano lililoandaliwa na Rais wa Oganaizesheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania, TPBO, Yassin Abdalla 'Ustaadh' litafanyika kwenye ukumbi wa Amana Club, Ilala jijini Dar.
Ustaadh aliiambia Micharazo kuwa, pambano hilo lisilo la ubingwa la raundi 12 ni maalum kwa ajili ya kupima viwango vya mabondia husika, pia kutoa fursa kwa mabondia wa mikoani kujitangaza kwenye mchezo huo.
Rais huyo wa TPBO, alisema Cobra ni bondia kutoka Arusha na hivyo kupata fursa ya kupigana na mkongwe Osward, kutampa nafasi ya kujitangaza katiuka mchezo huo.
Ustaadh alisema awali pambano hilo lilipangwa kufanyika Jumapili ijayo, ila kutokana na kuahirishwa kwa lingine la ngumi hizo za kulipwa kati ya Ashraf Suleiman na Awadh Tamim kutoka Machi 5 hadi Machi 12 imewafanya walisogeze mbele hadi Machi 20.
"Tumeona isingekuwa vema pambano letu lifanyika kama tulivyopanga Machi 13, wakati siku moja kungekuwa na pigano jingine la Ashraf na Tamim ambalo awali lilipangwa kufanyika Machi 5, lakini likasogezwa hadi Machi 12," alisema Rais huyo wa TPBO.
No comments:
Post a Comment