WIMBO mpya wa bendi ya Extra Bongo unatarajiwa kutambulishwa rasmi leo kwa mashabiki sambamba na vibao vingine na wanamuziki wapya uitwao, Mtenda Akitendewa umefyatuliwa video yake.
Video ya kibao hicho ambacho awali lilipangwa kufahamika kama 'Under 18' kimefyatuliwa na wanamuziki wa bendi hiyo wakiwa kambini kupitia kampuni ya Sophia Records ya jijini Dar es Salaam na utaanza kuonekana hewani wakati wowote kuanzia sasa.
Mkurugenzi wa Extra Bongo, Ally Choki 'Kamarade' aliiambia micharazo kuwa, waliamua kurekodi video ya wimbo huo wakiwa kambini kama njia ya kuwapa burudani mashabiki wao kuwaonyesha hawakuwa bure kambini bali walikuwa wakiwaandalia mambo mapya.
"Pamoja na kuandaa kazi mpya, lakini pia tumefyatua video ya moja ya vibao hivyo kiitwacho Mtenda Akitendewa ambacho kitaanza kuonekana wakati wowote,tumeshasambaza, kibao hicho na vingine pamoja na wanamuziki wapya tutawatambulisha rasmi Ijumaa (leo)," alisema.
Choki alisema onyesho la utambulisho kwa bendi yao utafanyika kwenye ukumbi wa New Msasani Club, ambapo kesho litafuatiwa na onyesho jingine TCC-Chang'ombe na kabla ya Jumapili kutambulishwa Mango Garden na kwenda kuvunja kambi yao ili kujiandaa kwenda Zanzibar.
Mtunzi na muimbaji huyo alizitaja nyimbo nyingine zitakazotambulishwa sambana na wanamuziki sita waliowanyakua wakienda kambini kutoka Twanga Pepeta ni Neema, Nguvu na Akili na Fisadi wa Mapenzi vinavyoandaliwa kwa ajili ya albamu mpya na ya pili.
Wanamuziki watakaotambulishwa kwenye maonyesho hayo ya mwishoni mwa wiki ni mtunzi na muimbaji nyota nchini, Rogert Hegga 'Caterpillar', Rapa Saulo John 'Ferguson', mpiga besi, Hoseah Mgohachi na wanenguaji Hassani Mohammed 'Super Nyamwela', Isaac Burhan 'Super Danger' na Otilia Boniface waliotoka African Stars 'Twanga Pepeta'.
No comments:
Post a Comment