STRIKA
USILIKOSE
Saturday, March 12, 2011
Talent wasubiri kidogo videoni
BENDI ya Talent 'Wazee wa Kuchechemea' imekamilisha kurekodi video ya nyimbo za albamu yao mpya ya 'Subiri Kidogo', huku ikiendelea kuandaa albamu ya pili.
Mkurugenzi wa bendi hiyo, Husseni Jumbe, alisema video ya albamu hiyo imekamilika mapema wiki hii na kwa sasa inafanyiwa uhariri kabla ya kusambazwa sokoni na kwenye vituo vya runinga.
Jumbe, alisema video ya albamu hiyo yenye nyimbo sita imetayarishwa na kampuni moja ya jijini na ina mandhari ya kuvutia ikirekodiwa kwa kiwango cha hali ya juu.
"Tumekamilisha kuiweka kwenye video albamu yetu mpya ya Subiri Kidogo, kwa sasa inahaririwa kabla ya kuanza kusambazwa ili mashabiki wetu wapate uhondo," alisema Jumbe.
Alizitaja nyimbo zilizorekodiwa kwenye video hiyo ni 'Subiri Kidogo', 'Dillema', 'Nyuma ya Pazia', 'Songombingo' na 'Nimeamua Kunyamaza'.
Jumbe alisema video hiyo ikikamilika, tayari bendi yake yenye wanamuziki 10, imeshaanza kuandaa albamu mpya ijayo.
Alisema nyimbo nne kati ya sita za albamu hiyo zimeshakamilika na kuanza kutambulishwa kwenye maonyesho yao ambazo ni pamoja na 'Shoka la Bucha', 'Jipu la Moyo' na 'Kilio cha Swahiba' ambao awali ulipangwa kuwepo kwenye albamu yao ya kwanza.
"Kibao cha Kilio cha Swahiba tuliamua kukiweka kwa ajili ya albamu hii ya pili, ambayo tayari ina nyimbo zingine tatu," alisema Jumbe.
Jumbe, alisema kabla ya Juni, albamu hiyo aliyopanga kuiitwa kwa jina la Shoka la Bucha huenda ikakamilika rasmi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment