STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, July 15, 2011

Twiga Stars kuanza na Ghana All African Games

SHIRIKISHO la Soka Afrika, CAF, imetangaza ratiba ya michuano ya soka kwa timu za wanawake zinazoshiriki michuano ya Afrika (All African Games) ambapo timu ya taifa ya Tanzania, Twiga Stars itaanza kibarua chake kwa kuumana na Ghana.
Michuano hiyo ya Afrika inatarajiwa kuanza kufanyika Septemba 3-18 kwenye mji wa Maputo, Msuimbiji, ambapo kwa mujibu wa ratiba hiyo ya CAF ni kwamba Twiga iliyopo kundi B itafungua dimba kwa kuumana na Ghana siku ya Septemba 5.
Timu zingine zilizopo katika kundi hilo ni Afrika Kusini na mabingwa wapya wa Kombe la COSAFA, Zimbabwe.
Ratiba hiyo ya CAF inaonyesha kuwa Twiga itashuka dimbani tena Septemba 8 kucheza na Afrika Kusini kabla ya kumaliza mechi zake, Septemba 11 kwa kucheza na Zimbabwe.
Twiga imejikuta kundi moja na timu hizo mbili ambazo ziliichachafya katika michuano ya Kombe la COSAFA, ambapo Afrika Kusini waliokuwa nao kundi moja waliwalaza bao 1-0 kabla ya Zimbabwe kuifunga kwenye mechi ya nusu fainali kwa mikwaju ya penati 4-2.
Timu zingine zitakazoshiriki michuano hiyo na zilizopangwa kundi A ni wenyeji Msumbiji, Cameroon, Algeria na Guinea, ambapo washindi wawili wa kwanza wa kila kundi ndizo zitakazosonga mbele kwa hatua ya nusu fainali.
Nigeria ndiyo waliokuwa mabingwa wa mwaka 2007, lakini hawakufanikiwa kufuzu
kwa michuano hiyo mwaka huu ambayo hufanyika kila baada ya miaka minne.
Wakati huo huo mikoa mitatu ya Dodoma, Mwanza na Ruvuma imeteuliwa kuwa vituo vya kuendeshea semina na mitihani ya utimamu wa mwili (physical fitness test) kwa waamuzi wa daraja la pili na tatu inayotarajiwa kufanyika mapema mwezi ujao.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Shirikisho la Soka Tanzania, TFF, kupitia Afisa Habari wake, Boniface Wambura, ni kwamba semina na mitihani hiyo itafanyika kwa muda wa siku tatu kuanzia Agosti 2-5 katika vituo hivyo.
Taarifa hiyo inasema washiriki wa semina na mitihani hiyo watajitegemea kila kitu kuanzia gharama za usafiri, chakula na malazi, huku vyama vya soka vya mikoa ya Tanzania Bara vikihimizwa kuwakumbusha washiriki kuhudhuria semina na mafunzo hayo kwa faida yao.
Iliongeza kuwa semina na mitihani hiyo itatumika kuwapandisha daraja washiriki hao.
Hiyo ni semina ya pili kuandaliwa na TFF ndani ya kipindi kifupi ikiwa ni maandalizi na msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara, kwani karibu wiki moja sasa ilikuwa ikiendesha semina kama hiyo inayowahusisha waamuzi wa daraja la IA na IB iliyokuwa ikifanyika katika miji ya Mwanza na Dar es Salaam.
Semina na mitihani hiyo ilianza Julai 13 na inatarajiwa kufungwa leo Julai 16.

No comments:

Post a Comment