STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, July 2, 2012

Yanga yakubali kwenda Zenji kushiriki Kombe la Urafiki

HATIMAYE timu ya soka ya Yanga imeamua kubadili msimamo wake wa kushiriki michuano ya Urafiki kwa kukubali kwenda visiwani Zanzibar kushiriki, ambapo inatarajiwa kuondoka leo sambamba na watani zao Simba. Awali uongozi wa Yanga 'ulichomoa' kushiriki michuano hiyo, lakini baada ya 'vikao' na waandaji wake, uongozi huo umelegea na kukubali kwenda kushiriki. Katibu Mkuu wa Yanga, Celestine Mwesigwa, alisema wamekubali baada ya kuridhiana na waandaaji na pia kwa vile michuano hiyo ina lengo la kudumisha urafiki baina ya timu za Tanzania Bara na Visiwani, hawakuona sababu ya kuigomea. "Tunaenda kushiriki, tutaondoka kesho asubuhi kuwahi michuano hiyo na tunaamini tutafanya vema na tutaaitumia kwa ajili ya fainali za Kombe la Kagame," alisema Mwesigwa. Mwesigwa alisema Yanga itaenda Zanzibar ikiwa na kikosi chake kamili ambacho Jumamosi iliitoa nishai Mabingwa wa Uganda, Express kwa kuilaza mabao 2-1 kwenye mechi ya kirafiki ya kimataifa iliyochezwa jijini Dar. Yanga ndio mabingwa watetezi wa michuano hiyo ya Kagame na itafungua dimba Julai 14 kwa kuumana na Atletico ya Burundi. Timu nyingine za Tanzania Bara zitakazoshiriki michuano hiyo ya Urafiki ni Simba ambao jioni ya leo inatarajiwa kushuka dimba la Amaan kuumana na Mafunzo.

No comments:

Post a Comment