Mpasuko wa kisiasa waibuka tena Zanzibar
Na Mwinyi Sadallah, Zanzibar
CHAMA cha Wananchi CUF kimesema kimegundua kuna viongozi wa SMZ hawataki maridhiano yaliyozaa serikali ya Umoja wa Kitaifa, Novemba mwaka 2010.
Tamko hilo limetolewa na Mkurugenzi wa habari, Uenezi na mawasiliano ya umma wa CUF jana Salim Bimani Abdalla, kufuatia vurugu zilizotokea katika uchaguzi mdogo wa jimbo la Bububu Septemba 16 mwaka huu.
Alisema kwamba chama hicho tayari kimewafahamu baadhi ya Viongozi kutoka CCM wanaopinga serikali ya Umoja wa kitaifa na tayari wanajitayarisha kuwashitakia kwa wananchi kupitia vyombo vya kutunga sheria Baraza la Wawakilishi Zanzibar (BLW) na Bungeni.
Alisema kwamba hatua hiyo itasadia wananchi kuwatambua viongozi wenye kinyongo na mabadiliko ya 10 ya Katiba ya Zanzibar ambayo yaliruhusu mfumo wa mpya wa serikali ya pamoja.
“Kuna Viongozi wa Serikali hawataki maridhiano yalioleta serikali ya Umoja wa kitaifa Zanzibar tumewafahamu kupitia uchaguzi wa Bububu,”alisema Bimani.
Alieleza kwamba vurugu za askari wa Vikosi kutumia nguvu kubwa ikiwemo kutisha watu kwa risasi za moto ni ushaidi wa kuwepo kuwepo viongozi ambao hawataki kubadilika na kumaliza siasa za uhasama visiwani humo.
Alisema kwamba hakutegemea vikosi vya SMZ kutumia nguvu kubwa ikiwemo kutumia risasi za moto kupiga hewani wakati Vikosi hivyo vipo chini ya Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais (IKULU).
Aidha alisema kwamba katika kampeni za uchaguzi huo kuna viongozi wa CCM walitumia majukwaa vibaya ikiwemo kutoa lugha za matusi dhidi ya viongozi wa CUF wanaoshiriki kuunda serikali ya Umoja wa kitaifa.
Akizungumzia tuhuma hizo Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai alisema tuhuma za CUF hazina msingi wowote na zimelenga kuficha ukweli na kuwadaganya wananchi.
Alisema kwamba chimbuko la vurugu katika uchaguzi huo limetokana na Viongozi wa CUF kupeleka Vijana 3000 usiku wa kuamkia uchaguzi na kuwapa kazi ya kutisha watu ikiwemo kuhakiki wapiga kura waliokuwa wanajitokeza wakiwa katika magari kinyume na sheria ya uchaguzi.
Vuai alisema kwamba vijana wa CUF walikuwa wakizuia watu kwenda kupiga kura hasa wafuasi wa CCM na kutoa vitisho kabla ya askari kuamua kuwatawanya katika maeneo ya vituo vya wapiga kura.
Vuai alisema kwamba wangalizi wa uchaguzi kutoka CUF wakiwemo mawaziri baadhi yao walifanya kazi kukagua kadi za wapiga kura wakati sio majukumu yao.
Alisema kwamba sheria za uchaguzi zilianza kuvunjwa mapema na baadhi ya Mawaziri wa CUF kutokana na kutumia magari ya umma wakati wa kampeni na uchaguzi kinyume na sheria na misingi ya Utawala bora.
Alisema kwamba CCM ilitarajia kuwa CUF watafanya kampeni za kistarabu baada ya kumaliza tofauti za kisiasa tangu kuuda serikali ya pamoja, lakini wameshindwa kubadilika na kuendeleza siasa za chuki na uhasama kinyume na mataraji ya wananchi.
Vuai alisema kwamba katika uchaguzi huo watu wenye asili ya Pemba awakuhojiwa uhalali wa kupiga kura tofauti na watu wenye asili ya Bambi, Makunduchi au Donge katika uchaguzi huo.
Vuai alisema akiwa kama muasisi wa muafaka kutoka CCM anajuta kwa kupoteza muda kutafuta amani ya Zanzibar baada ya kuibuka wanasiasa wanaorudisha siasa za chuki na ubaguzi na kuvuruga amani na Umoja wa kitaifa.
Alisema kwamba CUF imeshindwa kufanya siasa za kistarabu ikiwemo kukemea vitendo vya kuhatarisha amani na umoja wa kitaifa vinavyoofanywa na Jumuiya ya Uamsho na mihadhara Zanzibar. (JUMIKI).
Alisema Uamsho wamekuwa wakitoa lugha chafu dhidi ya Viongozi wa Kitaifa na waasisi wa muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
“Najuta kupoteza muda wangu kutafuta muafaka wa amani ya Zanzibar wakati wezetu awataki kuacha siasa za chuki na uhasama,’alisema Vuai ambaye alikuwa Mjumbe wa kamati ya Muafaka.
Alisema kwamba akukuwa na sababu za msingi kwa viongozi wa CUF kuhakiki kadi za wapiga kura katika vituo wakati ndani ya chumba cha wapiga kura kuna mawakala wa vyama na orodha ya majina ya wapiga kura yakiwa na majina na picha za wahusika.
Katika uchaguzi huo mgombea wa CCM Hussen Ibrahim Makungu aliebuka mshindi kwa kumtagulia mgombea wa CUF Issa Khamis issa ambaye amegoma kusaini matokeo na kutangaza kupiga matokeo mahakama Kuu ya Zanzibar.
Mwisho
No comments:
Post a Comment