Mapanga enzi za uhai wake |
UONGOZI wa bendi ya Msondo Ngoma 'Baba ya Muziki' umeeleza utaendelea kumlilia mpiga besi wao, Ismail Mapanga aliyefariki na kuzikiwa wiki iliyopita kwa madai ya amewaachia pengo.
Msemaji wa bendi hiyo, Rajabu Mhamila 'Super D' alisema marehemu Mapanga alikuwa mmoja wa wanamuziki tegemeo wa Msondo katika safu ya wacharaza magitaa.
Super D, alisema japo msiba ni kitu cha kawaida katika maisha ya wanadamu, lakini kwao Msondo kifo cha Mapanga kinawauma kutokana na mchango mkubwa ambao mwanamuziki huyo alikuwa akiutoa kwa bendi yao.
"Tutamlilia na kumkumbuka Mapanga, alikuwa mpiganaji ndani ya bendi kwa mchango wake, ametuachia pengo kubwa sio siri. Ni msiba mkubwa kwetu," alisema Super D.
Aidha, bendi yao inawashukuru wale wote kwa namna moja au nyingine walishiriki tangu mwanzo hadi mwisho katika msiba huo akidai Msondo haina cha kuwalipa zaidi ya kuwashukuru na kuwaombea kwa Mungu kwa walichokifanya.
"Tunawaombea kwa Mungu awalipe kwa walichokifanya na tunaiomba familia na ndugu jamaa wa marehemu wawe na uvumilivu katika kipindi hiki cha majonzi," alisema.
Mwanamuziki huyo aliyewahi kutamba na bendi na makundi mbalimbali ya sanaa likiwemo kundi la Muungano, alifariki Januari 23 kutokana na kuugua akiwa ziarani na Msondo mjini Tabora na kuzikwa siku iliyofuata jijini Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment