Salum Telela |
KIUNGO mkabaji wa klabu ya Yanga, Salum Telela ametangaza kuachana na soka kwa kile alichodai kukatishwa tamaa na hali ya majeruhi ya muda mrefu.
Nahodha huyo wa zamani wa timu ya taifa ya vijana U23, aliiambia MICHARAZO kuwa, ameona bora afanye shughuli nyingine ikiwamo kurejea shuleni kutokana na ndoto zake katika soka kukatishwa na majeraha yasiyopona.
Telela alisema jeraha lake la kifundo cha mguu kimekatisha ndoto zake kwa vile limeshindwa kupona licha ya juhudi kubwa zilizofanyika kujitibia na kuona ni bora sasa afanye mambo mengine na kusahau soka.
"Ndugu yangu nimeamua kuachana na soka kabisa kwa sasa kutokana na kuona hali ya majeraha kuniandama na kuchukua muda refu kupona," alisema.
Mchezaji huyo aliyewahi pia kung'ara Moro United na aliyetua Yanga ikiwa chini ya kocha Kostadin Papic na kuaminiwa katika kikosi cha timu hiyo alisema haoni sababu ya kuendelea na soka kama hapati nafasi ya kucheza.
"Kwa kweli nimekataa tamaa na soka, nilikuwa na ndoto nyingi katika mchezo huu lakini majeraha yamenifanya nichukue maamuzi haya magumu," alisema.
Kabla ya kuibukia Yanga na Moro United, Telela alilelewa kisoka na Shule ya Sekondari ya Makongo na kuonyesha makali yake akiwa pamoja na Omega Seme ambao waliaminiwa na kiocha Papic na kutamba timu za taifa za vijana.
Msimu uliopita aliichezea kwa mkopo Moro United iliyokuwa imerejea ligi kuu kabla ya kushuka tena na kurejeshwa Jangwani, msimu huu ambapo hakuweza kucheza mechi yoyote tangu Ligi Kuu ilipoanza Agosti mwaka jana.
Mwisho
No comments:
Post a Comment