STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, February 18, 2013

UCHAGUZI WA TFF WASIMAMISHWA,  KAMATI YA KUKUTANA LEO

Deogratias Lyatto, mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF
Na Boniface Wambura
KAMATI  ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imesitisha uchaguzi mkuu wa shirikisho hilo uliokuwa ufanyike Februari 24, huku mwenyekiti wake Deogratias Lyatto akikiri kwamba ni kweli yeye si mwanasheria kitaaluma kama ilivyoelezwa na mgombea aliyeengeuliwa katika nafasi ya makamu wa rais, Michael Wambura.
Akizungumza na waandishi wa habari, Lyatto alisema kuwa mchakato wa uchaguzi mkuu wa TFF na ule wa Bodi ya Ligi (PTL) uliokuwa ufanyike Februari 22 umesitishwa baada ya kamati ya uchaguzi anayoiongoza kubaini kuwa matatizo kadhaa ya kikanuni yanayotakiwa kutatuliwa kabla ya kuendelea na mchakato, ikiwamo muda mfupi kwa wagombea kuanza kampeni wakati kanuni zinataka kila mmoja wao apate zaidi ya siku tano kwa shughuli hiyo.

“Kamati ya uchaguzi ya TFF, kwa mamlaka iliyonayo kwa mujibu wa Ibara ya 10 (5) ya kanuni za uchaguzi za TFF, inasitisha zoezi zima la uchaguzi wa bodi ya TPL na TFF hadi hapo matatizo hayo ya kikanuni yatakapopata utatuzi,” alisema Lyatto.

Akielezea kuhusu madai ya Wambura kuwa kamati ya uchaguzi haina uhalali kwa vile mwenyekiti wake si mwanasheria kama katiba ya TFF inavyoelekeza, Lyatto alisema kuwa ni kweli yeye kitaaluma si mwanasheria, lakini kipengele hicho cha katiba kilitungwa wakati tayari akiwa na wadhifa huo.

Akaeleza zaidi kuwa rais mpya atakayechaguliwa kuongoza ndiye atakayekuwa na mamlaka pekee ya kuteua mtu mwingine mwenye sifa zilizoelekezwa kwenye katiba.

Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF, Idd Mtiginjola, amesema kuwa leo saa 5:30 asubuhi wataanza kusikiliza maombi ya kupitia upya maamuzi ambayo iliyatoa kuhusu rufani ilizoziamua dhidi ya wagombea na wawekapingamizi na kwamba, wakati wa kufanyika kwa zoei hilo, kila mdau anaruhusiwa kuhudhuria wakiwamo wahusika, mawakili na hata waandishi wa habari.

Miongoni mwa waliotuma maombi ya kutaka kupitiwa upya kwa maamuzi ya kamati ya rufaa ni aliyekuwa mgombea wa nafasi ya urais kabla ya kuenguliwa na kamati hiyo, Jamal Malinzi na mgombea wa uenyekiti wa Bodi ya Ligi, Ahmed Yahya

No comments:

Post a Comment