Kikosi cha Kagera Sugar |
KIVUMBI cha Ligi Kuu Tanzania Bara kinatarajiwa kuendelea tena kesho nchini, huku pambano la jijini Dar es Salaam kati ya vinara Yanga dhidi ya wageni wao Kagera Sugar ni kama vita vya kulipizana kisasi.
Yanga inayoongoza msimamo wa ligi hiyo ikiwa imejiukusanyia pointi 39 itaikaribisha Kagera kwenye uwanja wa Taifa, ikiwa na kumbukumbu ya kipigo cha bao 1-0 ilichopewa katika mechi ya mzunguko wa kwanza walipoenda mjini Kagera.
Kikosi cha Yanga |
Kadhalika Yanga itashuka dimbani ikiamini kuteleza mbele ya Kagera ni kutoa mwanya wa Azam waliopo nafasi ya pili ambao hawatakuwa uwanjani kwa kesho kwa vile wanaenda Sudan Kusini kuvaana na Al Nasir Juba, kuja kuwasogelea katika mbio zao za kuwania ubingwa wa ligi hiyo msimu huu.
Azam yenyewe wapo nafasi ya pili na pointi zao 36, huku Simba wanaoshikilia taji hilo kwa sasa wakiwa nafasi ya tatu na pointi 31, ambazo huenda zikapitwa kesho na Coastal Union itakayoikaribisha Ruvu Shooting kwenye uwanja wa Mkwakwani Tanga.
Kagera inayonolewa na mshambuliaji nyota wa zamani wa Majimaji Songea, Simba na Taifa Stars, Abdallah King Kibadeni, siyo timu ya kubezwa, japo rekodi zinaoonyesha inapocheza na Yanga nje ya uwanja wao wa nyumbani huwa haina madhara kama wakiwa Kaitaba.
Kikosi cha Kagera kinashika nafasi ya tano kikiwa na pointi 28 na ushindi wowote kwao utaifanya ilingane pointi na Simba, lakini pia kujiweka katika mazingira mazuri ya kuingia kwenye Nne Bora.
Rekodi kwa timu hizo mbili kwa misimu mitatu kuanzia ule wa 2010, unaoonyesha Yanga imeshinda mara tatu na kupoteza mara mbili.
Msimu wa 2010 Yanga walishinda mechi zote mbili nyumbani na ugenini, ikiifunga Kagera jijini Dar mabao 2-0 katika mechi iliyochezwa Septemba, 22 na kuendeleza ubabe mjini Kagera kwa kuilaza Kagera bao 1-0 mechi iliyopigwa Februari 16, 2011.
Katika msimu uliopita, Yanga ilipata ushindi nyumbani Oktoba 14, 2011 kabla ya kwenda kulala katika mechi ya marudiano mjini Kagera iliyochezwa Machi 18, 2012 na msimu huu ilipata kipigo cha bao 1-0 mjini Kagera Oktoba 7, 2012 na haijulikani kesho nani ataibuka mshindi?
Mwechi nyingine zitakazochezwa kesho mbali na Yanga na Kagera na ile ya Coastal Union dhidi ya Ruvu Shooting, pia Mtibwa Sugar itakuwa nyumbani kuuikaribisha Prisons ya Mbeya, Polisi Moro itaialika Mgambo JKT na JKT Ruvu itaikaribisha Toto African uwanja wa Chamazi Complex, Dar es salaam.
No comments:
Post a Comment