STRIKA
USILIKOSE
Monday, March 11, 2013
Simba yakana kuwasimamisha wachezaji wake
Na Ezekiel Kamwaga
JANA na leo, zimetolewa habari tofauti kuhusiana na klabu ya Simba ambazo uongozi umeona ni vema uzitolee ufafanuzi kwa lengo la kuweka rekodi sawa. Ufuatao ndiyo ufafanuzi wa taarifa hizo.
1. SIMBA KUZUIWA HOTELINI
SAA mbili kabla ya mechi ya jana baina ya Simba na Coastal Union ya Tanga, mmiliki wa Saphire Court Hotel alitoa taarifa kwa uongozi wa Simba kwamba ataizuia timu isiondoke hotelini kwa vile anaidai Sh milioni 25 na anataka alipwe zote jana.
Ikumbukwe kwamba Simba imekuwa ikikaa hotelini hapo kwa muda mrefu sasa wakati inapoweka kambi. Pia, wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya Simba walifanya mkutano na wachezaji wote wa Simba katika hoteli hiyo usiku wa kuamkia jana.
Wamiliki wa hoteli hiyo hawakutoa taarifa yoyote kwa uongozi wakati huo juu ya dhamira yao hiyo.Wamiliki hao hawakutoa taarifa asubuhi ya mechi na walisubiri mpaka wakati timu inataka kuondoka ndiyo wakachukua hatua hiyo.
Kwa uongozi wa Simba, hatua hiyo ilikuwa ya ghafla mno. Ifahamike kwamba kabla ya hatua hiyo, uongozi wa Simba ulikuwa umemlipa mmiliki huyo kiasi cha zaidi ya Sh milioni 30 katika kipindi cha miezi 10 iliyopita.
Mara baada ya mechi dhidi ya Libolo ya Angola, Saphire walilipwa Sh milioni 15 na Simba. Hii maana yake ni kwamba klabu yetu ina utaratibu wa kulipa madeni yake na si watu wasiolipa kama hatua hiyo ya wamiliki wa Saphire inavyotaka kueleza.
Uongozi wa Simba tayari ulitoa ahadi ya kumaliza deni lote inalodaiwa baada ya kulipwa fedha zake inazodai zinazotakiwa kulipwa wakati wowote mwezi huu au ujao.
Simba inadai zaidi ya Sh milioni 500 kwa wadai wake wawili (Etoile du Sahel ya Tunisia na Push Mobile) na inataraji kulipwa fedha hizo. Itakapolipwa fedha zake hizo, Simba itakuwa na uwezo wa kulipa madeni yake yote inayodaiwa na watu binafsi na makampuni bado ikabaki na fedha za kufanya mambo mengine ya kimaendeleo.
Wakati ikisubiri ilipwe fedha zake inazodai, Simba itaendelea kulipa madeni yake taratibu kwa kadri itakavyoweza. Ifahamike kwamba kwa sasa chanzo kikuu cha mapato ya klabu ni fedha za mapato ya milangoni na za udhamini wa bia ya KILIMANJARO ambazo hazikidhi mahitaji yote ya timu.
Kwa kuzingatia nakisi hii ya mapato na matumizi, Simba SC imeanza mchakato wa kutafuta wafadhili na wadhamini kokote walipo duniani ili kuongeza mapato yake.
Tayari mawasiliano yameanza na wenzetu wa Sunderland ya England kupitia mradi wao wa Invest in Africa ili Simba nayo ifaidike. Simba SC inaomba pia umma ufahamishwe kwamba klabu ya soka kudaiwa si dhambi.
Iwapo klabu kubwa na tajiri duniani kama vile Manchenster United, Real Madrid na Liverpool zina madeni, inakuaje madeni ya Wekundu wa Msimbazi (tena ambayo klabu ingeweza kuyalipa yote iwapo wadeni wake nayo wangewalipa kwa wakati) yaonekane kama kitu kigeni?
Uongozi unaahidi kwamba utalipa madeni yake yote kwa kadri utakavyojaaliwa. Kwenye lugha ya kibenki, credit worthiness ya mteja inamaanisha mteja ambaye anakopa na kulipa. Simba inapenda kusisitiza kwamba ni taasisi ya kuaminika na yenye heshima kubwa na bado inavutia watu na taasisi mbalimbali za ndani na nje ya nchi. Simba ni CREDIT WORTHY INSTITUTION !
Hata hivyo, uongozi wa Simba unafikiria kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wamiliki wa Saphire Court Hotel kwa kitendo chake cha kuwazuia wachezaji na viongozi wa Simba hotelini kabla ya mechi ya jana. Simba inachukulia kitendo kile kama hujuma na kisheria kinaangukia katika kundi la FORCED IMPRISONMENT kwa wamiliki kuwazuia watu kinguvu hotelini kwao.
Wamiliki hawakutoa notisi kwa uongozi au taarifa yoyote ya mdomo au maandishi kabla ya kuchukua hatua hiyo. Lengo lilikuwa ni kuchafua heshima na hadhi ya Simba kwa hoteli ambayo imetoka kulipwa Sh. milioni 15 wiki mbili tu zilizopita.
Uongozi wa Simba SC unaapa kuilinda na kuitetea hadhi ya klabu yetu kwa nguvu zetu zote, akili zetu zote na maarifa yetu yote.
2. WACHEZAJI, BENCHI LA UFUNDI KUFUKUZWA
KUNA taarifa zimeenezwa pia kwamba kuna wachezaji wa Simba wamesimamishwa au kufukuzwa kuchezea Simba.
Habari hizi nazo hazina ukweli wowote Ukweli ni kwamba, uongozi wa Simba umetoa ruksa kwa benchi la ufundi kupanga timu ambayo litaona inafaa kwa mechi husika.
Uongozi hautaingilia, kwa namna,njia au aina yoyote ile utendaji wa benchi la ufundi. Hakuna mchezaji yeyote aliyesimamishwa hadi sasa.
Pia uongozi unakanusha taarifa kuwa Daktari Mkuu wa Klabu, Cosmas Alex Kapinga, kuwa naye ameachia ngazi. Habari hizi hazina ukweli kwani daktari huyo ana ruhusa ya kikazi ya wiki mbili inayojulikana.
HITIMISHO
Katika namna ya kipekee kabisa, uongozi wa Simba unapenda kutoa shukrani za dhati kabisa kwa washabiki wake waliojitokeza Uwanja wa Taifa na kuisapoti timu kwa asilimia 100.
Uongozi unathamini sana mchango wa wanachama wake na unaahidi kufanya kila unachoweza kuwarejeshea tena furaha mioyoni mwao.
Pia unatumia nafasi hii kuwapongeza wachezaji na benchi la ufundi ambao walicheza mechi ya jana katika mazingira magumu. Walicheza bila ya kufanya warm up na wakitoka kuwa wamezuiwa hotelini jambo ambalo lingeweza kuwaondoa mchezoni.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment