Kikosi cha Azam |
CHAMA cha Soka Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) kimetoa wito kwa mashabiki wa soka jijini na mikoa ya jirani kufurika kwa wingi kwenye Uwanja wa Taifa leo kushangilia Azam katika pambano la Kombe la Shirikisho la klabu za Afrika.
Azam inatarajiwa kuvaana na Barrack YCII ya Liberia katika pambano la marudiano la raundi ya kwanza ya michuano hiyo wakiwa wawakilishi pekee wa nchi katika michuano ya kimataifa.
Katika pambano la awali lililochezwa ugenini mjini Monravia, Liberia Azam ilishinda 2-1 hivyo leo kuhitaji hata kutofungwa zaidi ya 1-0 ili kuingia raundi ya pili ya michuano hiyo ya pili kwa ukubwa kwa ngazi za klabu Afrika.
Ili kuhakikisha Azam inafuzu hatua hiyo, DRFA imewaomba wadau wa soka kujitokeza kwa wingi ili kuipa sapoti timu hiyo, mbali na kuwataka wachezaji wa klabu hiyo kupigana uwanjani kuwapa ushindi wawakilishi hao.
Katibu Mkuu wa DRFA, Msanifu Kondo aliiambia MICHARAZO kuwa anaamini kucheza uwanja wa nyumbani na kushangiliwa na mashabiki wake ni faida kubwa ya kuisaidia Azam kushinda hivyo mashabiki wasisite kujitokeza uwanjani.
"DRFA tunawaomba mashabiki wa soka bila kujali itikadi zao wajitokeze kwa wingi uwanja wa Taifa kwa ajili ya kuipa sapoti Azam itakapokuwa ikirudiana na Barrack ya Liberia," alisema Kondo.
Azam ilipata fursa ya kucheza raundi ya kwanza baada ya kuing'oa Al Nasir Juba ya Sudan Kusini kwa jumla ya mabao 8-1.
No comments:
Post a Comment