STRIKA
USILIKOSE
Tuesday, April 9, 2013
Superspot yapangua ratiba ya Ligi Kuu Tanzania Bara
RATIBA ya mechi za Ligi Kuu ya Tanzania Bara imefanyiwa marekebisho mbalimbali ambapo baadhi ya mechi hizo zimesogezwa mbele zikiwamo zinazozihusu klabu za Simba na Yanga.
Mechi baina ya Yanga na JKT Oljoro iliyokuwa ichezwe kesho Jumatano itapigwa Jumamosi Aprili 13 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam wakati mchezo unaosubiriwa kwa hamu baina ya Azam na Simba uliokuwa ufanyike Jumamosi ya Aprili 13 sasa utakuwa Jumapili (Aprili 14) kwenye uwanja huo huo.
Mabadiliko hayo yanalenga kutoa nafasi kwa mechi hizo za Ligi Kuu ya Bara kuonekana moja kwa moja katika kituo cha televisheni cha kulipia cha Super Sport chenye lengo cha kuja kuidhamini ligi hiyo.
Akizungumza jana jijini, Afisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura, alizitaja mechi nyingine zilizofanyiwa marekebisho katika ligi hiyo kuwa ni Azam dhidi ya African Lyon sasa watachuana Alhamisi kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi badala ya kesho.
Wambura alisema mchezo mwingine uliosogezwa mbele ni kati ya Mgambo JKT dhidi ya Yanga ambao sasa utafanyika Aprili 17 mwaka huu badala ya Jumamosi kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
Aliitaja mechi nyingine itakayorushwa hewani kuwa ni ya Coastal Union dhidi ya JKT Ruvu itakayochezwa Aprili 16 badala ya Aprili 10 na kuongeza kuwa mchezo mwingine uliofanyiwa marekebisho ni kati ya Mtibwa Sugar dhidi ya JKT Oljoro ambao sasa utafanyika Aprili 17 badala ya Aprili 13.
Aliongeza kuwa mechi nyingine zitabaki kama zilivyopangwa awali ikiwamo ya Yanga dhidi ya Simba itakayofanyika siku ya funga dimba ya ligi hiyo kwa timu zote 14 zinazoshiriki ligi hiyo kushuka dimbani.
Hata hivyo, afisa habari wa Yanga, Baraka Kizuguto alisema jioni jana kuwa wamepeleka barua TFF ya kupinga mabadiliko hayo kwa kuwa yameganyika bila ya kuwashirikisha.
Yanga wanaongoza ligi hiyo kwa pointi 49 wakifuatiwa na Azam wenye pointi 43, Kagera Sugar (pointi 37) na mabingwa watetezi Simba walio katika nafasi ya nne kwa kuwa na pointi 35.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment