Nsa Job (kulia) |
Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah |
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Katibu mkuu wa TFF, Angetile Osiah, alisema katika barua yao waliyomuandikia mshambuliaji huyo hawakumpa siku maalumu lakini endapo nyota huyo atachelewa kujisalimisha atakumbushwa kabla ya kuchukuliwa hatua kupitia kamati husika.
"Tuliiweka wazi lakini tutamuandikia barua nyingine ya kumkumbusha na itakayofuata itakuwa imetoa muda fulani, ila tunaamini atatoa ushirikiano kama alivyokaririwa na gazeti (la NIPASHE)," alisema Katibu mkuu huyo.
Osiah alisema TFF inaamini mchezaji huyo atatoa ushirikiano kama alivyolieleza gazeti la NIPASHE lilipozungumza naye mapema wiki hii.
Aliongeza kwamba wanaamini akiwa wazi mhusika wa tuhuma hizo atajulikana na hatimaye adhabu itatolewa na kukomesha suala la rushwa katika soka la nchini.
Osiah alisema pia tayari Mkurugenzi wa Vipindi wa kituo cha redio cha Clouds ameahidi kuwapa ushirikiano katika kupata nakala ya kipindi kilichorushwa mahojiano na Nsa ambacho kilifanyika Aprili 3 mwaka huu.
Nsa alizungumza katika mahojiano na kituo cha redio hiyo akisema aliwahi kupokea rushwa lakini aliifungia timu yake goli pekee la ushindi.
Hata hivyo, hadharani, hakuitaja timu aliyokuwa anaichezea wakati huo wala timu aliyoifunga na wala jina la kiongozi aliyemhonga, ambaye alisema alianza kumsumbua kudai fedha zake pale “alipowatungua”.
Nyota huyo ambaye kwa sasa anafanya mazoezi binafsi baada ya kufanyiwa upasuaji wa goti nchini India aliwahi kuchezea timu za Simba, Yanga, Moro United, Azam, Villa Squad na sasa Coastal Union zote zinazoshiriki Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
Nsa aliiambia NIPASHE kwamba atatoa ushirikiano kwa TFF kama alivyotakiwa na kwa sasa anajiandaa kwenda kukutana nao.
Alisema pia alipokea barua hiyo tangu wiki iliyopita na atafanya kila linalowezekana ili kutekeleza kile atakachoambiwa na wajumbe wa kamati hiyo.
CHANZO:NIPASHE.
No comments:
Post a Comment