STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Wednesday, April 17, 2013

Yanga kuvuna nini kwa Mgambo, Toto kujishusha daraja?





VINARA wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga leo watakuwa Mkwakwani Tanga kukabiliana na wenyeji wao Mgambo JKT, akili zao zikiwa kwenye taji la ubingwa ambalo kwa sasa halina mwenyewe baada ya Simba kulitema wiki iliyopita.
Yanga inahitaji pointi tano tu katika mechi zake nne zilizosalia kabla ya kumalizika kwa msimu wa 2012-2013 kutangazwa kuwa bingwa, na tayari wameapa kwamba leo ni lazima Mgambo walegee kwao kabla ya kuwakabili JKT Ruvu Jumapili kwenye uwanja wa Taifa.
Ingawa leo kuna mechi nyingine mbili, ikiwamo iliyo katika hatia hati ya kuchezwa kati ya Kagera Sugar dhidi ya Toto African, macho na masikio ya mashabiki wa soka yapo Mkwakwani kutaka kusikia na kuona kama Yanga itaendeleza rekodi yake ya kutopoteza mechi yoyote ndani ya mwaka 2013.
Yanga imeapa kuvuna pointi tatu katika pambano hilo litakalochezeshwa na mwamuzi Athuman Lazi kutoka Morogoro atakayesaidiwa na Michael Mkongwa wa Iringa na Godfrey Kihwili kutoka Arusha na kamishna wa mchezo huo anatarajiwa kuwa Godbless Kimaro kutoka Moshi, ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kuwa bingwa mpya wa Tanzania na kutwaa taji la 23 katika ligi hiyo tangu mwaka 1965.
Kocha wa  Ernie Brandts, alinukuliwa jana kuwa mchezo huo wa leo, utamwongezea asilimia 10 kati ya 90 alizokuwa nazo za kutwaa ubingwa na kudai kuwa awali alitishwa na kasi ya wapinzani wao Azam ambao Jumapili iliyopita walisimamishwa na Simba kwa kutoka sare ya mabao 2-2.
Licha ya kujipa asilimia hizo endapo watashinda mchezo huu, amewataka vijana wake kutokuwa na papara ili kuhakikisha wanashinda na kutimiza malengo yao kabla ya ligi kuisha.
Hata hivyo Yanga itawakabili Mgambo bila baadhi ya nyota wake ambao ni majeruhi na wengine wagonjwa akiwamo kiungo mahiri, Haruna Niyonzima, beki Juma Abdul na mshambuliaji Didier Kavumbagu.
Afisa Habari wa Yanga, Baraka Kizunguto alitamba kuwa licha ya kuwakosa nyota hao bado Yanga wapo imara kuweza kuvuna pointi tatu ili kuwaweka karibu na ubingwa na kuikimbia Azam waliopo nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi hiyo ambao watakuwa 'likizo' kujiandaa na pambano la kimataifa dhidi ya FAR Rabat ya Morocco katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Ukiondoa pambano la Mkwakwani, jioni ya leo pia kutakuwa na mechi nyingine zinazohusisha timu ndugu za Mtibwa Sugar na Kagera Sugar ambazo zitakuwa viwanja vyao vya nyumbani kuzikaribisha JKT Oljoro na Toto African, japo Toto imesisitiza kuwa haitakwenda Kagera kuumana na Kagera Sugar leo.
Katika pambano la Manungu, Mtibwa na Oljoro zitahukumiwa na mwamuzi Israel Mkongo, ambapo wenyeji watakuwa wakisaka ushindi utakaowawezesha kuchupa hadi nafasi ya tano baada ya jana kuenguliwa na Coastal baada ya kuambulia sare ya 0-0 mbele ya maafande wa JKT Ruvu.
Yanga ina pointi 52, ikifuatiwa na Azam pointi 47, Kagera Sugar pointi 37, kisha kufuatiwa Simba yenye pointi 35 na kufuatiwa na Coastal na Mtibwa zenye pointi 33 kila mmoja na kutofautiana kwenye uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa.

No comments:

Post a Comment