STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, May 10, 2013

Vita tupu Dar, Kagera katika Ligi Kuu kesho


Kagera Sugar Fc
Azam Fc
Mgambo JKT

Ruvu Shooting Stars
Na Boniface Wambura
Kagera Sugar inaikaribisha Ruvu Shooting ya Pwani katika mchezo pekee wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) utakaofanyika kesho (Mei 11 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Kaitba mjini Bukoba.

Ingawa timu zote mbili hazipambani kutafuta ubingwa ambao tayari umetwaliwa na Yanga wala kukwepa kushuka daraja, mechi hiyo bado ni muhimu kwao katika mazingira matatu tofauti.

Kagera Sugar inayonolewa na kocha mkongwe kuliko wote katika VPL, Abdallah Kibaden na ikiwa na pointi 40 yenyewe inasaka moja kati ya nafasi nne za juu ambazo zina zawadi kutoka mdhamini wa ligi, lakini pia timu zinazoshika nafasi hizo za juu zinapata tiketi ya kucheza michuano ya BancABC Super 8.

Kwa upande wa Ruvu Shooting ya Kocha Charles Boniface Mkwasa yenye pointi 31 inasaka moja ya nafasi sita za juu ambazo ni fursa ya kuingia kwenye Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPL Board) ambayo inatarajiwa kuundwa baada ya uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Septemba 28 mwaka huu.

Wagombea nafasi za uenyekiti na makamu wake ni lazima watoke katika timu zilizoshika nafasi sita la juu katika VPL msimu uliopita. Uchaguzi wa TPL Board utafanyika siku moja kabla ya ule wa TFF uliopangwa kufanyika Septemba 29 mwaka huu.

Raundi ya 25 ya ligi hiyo itakamilika keshokutwa (Mei 12 mwaka huu) kwa mechi kati ya wenyeji Azam na Mgambo Shooting ya Tanga. Mechi hiyo namba 169 itachezwa katika Uwanja wa Azam Complex ulioko Chamazi, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.

Azam yenye pointi 48 inahitaji moja zaidi ili kutetea nafasi yake ya umakamu bingwa iliyoutwaa msimu wa 2011/2013 na kupata tiketi ya kuiwakilisha Tanzania katika mashindano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika.

Wakati Azam ikisaka pointi hiyo moja, Mgambo Shooting inayofundishwa na wachezaji wa zamani wa mabingwa wa Tanzania Bara mwaka 1988, Mohamed Kampira akisaidiwa na Joseph Lazaro ni moja ya timu ziko katika hatari ya kurudi Ligi Daraja la Kwanza (FDL) msimu ujao.

Mgambo Shooting inahitaji pointi moja tu katika mechi mbili ilizobakiza kukwepa kurudi FDL, ikishindwa kupata pointi hiyo huku Polisi Morogoro na Toto Africans ya Mwanza zikishinda mechi zao za mwisho kwa uwiano mzuri wa mabao itakuwa imekwenda na maji.

Mechi ya Azam dhidi ya Mgambo Shooting itachezeshwa na refa Jacob Adongo kutoka Mara, na atasaidiwa na Abdallah Rashid wa Pwani na Charles Mbilinyi wa Mwanza. Mwamuzi wa mezani atakuwa Idd Lila wa Dar es Salaam wakati Kamishna ni Omari Walii wa Arusha.

No comments:

Post a Comment