Oscar Joshua |
Joshua, aliyetwaa taji la ligi kuu mara mbili sawa na idadi ya Kombe la Kagame akiwa na Yanga, alisema ugumu wa ligi hiyo unaweza kuonekana katika matokeo ya kushangaza katika mechi zilizochezwa mpaka sasa.
Akizungumza na MICHARAZO katika mahojiano maalum, beki huyo alisema kwa mfano Yanga iliweza kuitungua Ashanti United magoli 5-1, lakini timu hiyo hiyo iliweza kuisimamisha Azam ambayo waliicharaza Yanga mabao 3-2.
"Kwa ligi ya msimu huu ni ngumu sijawahi kuona, inasisimua na inafanya iwe vigumu mtu kutabiri nani atakayeibuka na ubingwa kwa sababu hakuna timu nyonge kama ilivyokuwa misimu kadhaa iliyopita," alisema Joshua.
Beki huyo mwenye 'mwili jumba', alisema anadhani kuwepo kwa udhamini wa uhakika na vijana wengi kupewa nafasi katika timu shiriki zimesaidia kuifanya ligi iwe na ushindani na upinzani mkubwa.
Alisema kuwepo kwa ligi ngumu kama hiyo itasaidia kuliweka soka la Tanzania katika kiwango kizuri na hatiamye kupatikana kwa timu nzuri ya taifa itakayoipeperusha vyema bendera katika anga la kimataifa.
Joshua aliizungumzia timu yake ya Yanga ambao ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu kuwa, pamoja na kwamba imeonekana kuyumba, lakini bado anaamini italitetea taji lake mwisho wa msimu.
"Kwa sasa tupo nafasi ya nne, lakini hii haitukatishi tamaa kwa sababu tumejipanga kupigana mpaka mwisho kuhakikisha tunalitetea taji kwa mara ya pili, licha ya kutambua kuna upinzani mkali toka kwa wengine," alisema.
No comments:
Post a Comment