Na Boniface Wambura
KIONGOZI
wa Mbio za Mwenge wa Uhuru, Juma Ali Amir amefungua kituo cha kwanza
cha Football for Hope kilicho mkoani Iringa kwa kuwataka wananchi
kukituia vizuri ili wanufaike na huruma za kijamii zinazotolewa na
taasisi ya IDYDC pamoja na kuendeleza mpira wa miguu.
Akizungumza
wakati wa uzinduzi wa kituo hicho jana (Oktoba 13 mwaka huu), kiongozi
huyo amesema taasisi ya IDYDC (Iringa Development of Youth, Disabled and
Child Care) wamefanya vizuri kuamua kutumia mpira wa miguu kusaidia
jamii kwa kuelimisha juu ya mambo mbalimbali kama ugonjwa wa ukimwi,
kusaidia walemavu, haki za watoto na afya ya jamii.
Naye
Mwakilishi wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), Patrick
Onyango amesema amefurahishwa na kukamilika kwa kituo ambacho
kitasaidia jamii.
Amesema
idadi kubwa ya watu waliofika kwenye uzinduzi huo inadhihirisha ni
kiasi gani kituo hicho kitakuwa na matokeo mazuri kwa jamii.
Onyango
alisema hicho ni kituo cha 14 kukamilika kati ya 20 vinavyojengwa
barani Afrika ikiwa ni mpango wa FIFA kurudisha kwa jamii mafanikio
iliyopata kwenye fainali za kwanza za Kombe la Dunia barani Afrika.
Kituo hicho kina uwanja mdogo wa mita 20 kwa 40 uliowekwa nyasi bandia, jengo lenye ukumbi wa mikutano kwa ajili ya semina, chumba cha kupimia ukimwi, chumba cha ushauri nasaha, maktaba na ofisi.
Zaidi ya dola 270,000 za Marekani zimetumika kukamilisha ujenzi wa kituo hicho kilicho eneo la Mtwivila, Iringa mjini.
No comments:
Post a Comment