STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Thursday, October 31, 2013

Rais JK kushiriki mbio za Uhuru Marathon

Rais Jakaya Kikwete

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Kikwete anatarajiwa kushiriki katika mbio maalum za Uhuru (Uhuru Marathon) zitakazofanyika Desemba 8 jijini Dar es Salaam imefahamika.
Mshindi wa jumla wa mbio hizo za marathoni (kilomita 42) atakabidhiwa zawadi ya Sh. milioni 3.5.
Akizungumza jana kwenye ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Katibu Mkuu wa kamati ya maandalizi ya mbio hizo, Innocent Melleck, alisema kuwa Rais Kikwete atakabidhiwa fomu namba moja ya kujisajili katika ushiriki wa mbio hizo huku akimtaja Spika wa Bunge, Anne Makinda kuwa atapewa fomu namba mbili.
Melleck alisema kuwa viongozi hao watashiriki mbio za kilomita tatu na kumtaja mshiriki mwingine wa mbio hizo ni Kiongozi wa Kambi ya Upinzani bungeni na Mbunge wa Jimbo la Hai, Freeman Mbowe.
Alisema kuwa tayari fomu za kujiandikisha zimeanza kutolewa katika vituo mbalimbali nchini jana huku zoezi hilo likitarajiwa kufanyika kwenye viwanja vya Bunge mkoani Dodoma Jumanne na Jumatano wiki ijayo.
Alisema ada ya fomu hizo kwa mbio za marathoni ni Sh. 6,000 huku za kilomita tano zikiwa ni Sh. 2,000 na zitashirikisha pia wanariadha kutoka nje ya nchi.
Alieleza kuwa lengo la kuanzisha mbio hizo ni kutaka kuenzi na kudumisha amani iliyopo nchini na kukumbushana kutochezea thamani hiyo.
"Kupitia mbio hizi tutaweka tofauti zetu pembeni, Tanzania kwanza, Amani Kwanza," alisema katibu huyo wa kamati ya maandalizi.
Aliwataka wadau na taasisi mbalimbali kujitokeza kudhamini mbio hizo zitakazokuwa zinafanyika kila mwaka nchini.

No comments:

Post a Comment