STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Sunday, October 20, 2013

Simba yafanya maajabu Taifa, Ngassa aokoa nyumba zake


Mrisho Ngassa akishangilia bao lake leo uwanja wa Taifa

MRISHO Ngassa ameziokoa nyumba zake zisichomwe moto, lakini Yanga wameshindwa kulinda ushindi wao wa mabao matatu kama walivyoahidi baada ya Simba kuchomoa mabao na kulazimisha sare ya mabao 3-3.
Wapinzani hao wa jadi waligawana utawala wa vipindi, Yanga ikitawala kipindi cha kwanza na kujipatia mabao yake matatu kupitia kwa Mrisho Ngassa na Hamis Kiiza 'Diego' kabla ya Simba kung'ara kipindi cha pili.
Mabao ya Betram Mombeki na mabeki wa kimataifa Joseph Owino na Gilbert Kazze yalizima ndoto za Yanga kuwanyuka watani zao kwa mara ya pili mfululizo.
Pambano hilo lililosisimua wengi lililochezwa kwenye uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam limeisaidia tu Yanga kupanda nafasi moja toka ya tano hadi ya nne ikiishusha Mtibwa Sugar, huku Simba ikishindwa kurejea kileleni.
Sare hiyo imeifanya Simba ifikishe pointi 19, moja dhidi ya vinara Azam na Mbeya City ambazo jana zilitakata kwa ushindi wa bao 1-0 kila mmoja dhidi ya timu za maafande wa JKT Ruvu na Oljoro JKT.
Kwa ujumla Yanga itawabidi wajilaumu kwa matokeo hayo kwani ilikuwa na kila dalili za kuweza kulipa kisasi cha mabao 5-0 iliyopewa na Simba Mei mwaka jana na hata kurudisha bao 6-0 iliyofungwa miaka 36 iliyopita.
Kipindi cha kwanza iliwashika Simba na kucheza watakavyo hasa baada ya kiungo cha Simba 'kufa', lakini walionyesha kuridhika huku Simba kutumia muda wa mapumziko kurekebishana makosa na kujirekebisha.
Kuingia dimbani kwa Said Ndemla na William Lucian 'Gallas' walifanya Simba ipate uhai na kutawala kipindi cha pili na kuwafunika Yanga ambao walionekana kuridhika na kudhani wameshashinda mchezo huo.
Baadhi ya mashabiki wa soka wameonyesha kushangazwa na matokeo ya leo Yanga wakilaumiana na wachezaji wao, huku Simba wakishangilia, japo makocha wote wametoa lawama kwa wachezaji kwa jinsi walivyocheza.
King Kibadeni ameweka wazi kwamba katika kikosi chao kuna tatizo kubwa japo hakupenda kuweka bayana, huku Ernie Brandts akidiriki 'kuwatusi' wachezaji wake kwa kuruhusu mabao matatu kurudi.

Lakini kubwa ni kitendo cha Ngassa kufunga bao na kutimiza ahadi yake aliyotoa kwamba kama asingefunga au kutoa pasi ya bao basi angechoma moto nyumba zake tano.

No comments:

Post a Comment