STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Wednesday, October 23, 2013

Yanga 'yaua' Taifa, Mnyama abanwa Tanga, Kiiza hashikiki


MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga imesahihisha makosa yake leo kwa kuicharaza Rhino Rangers ya Tabora kwa mabao 3-0 wakati Simba ikilazimisha suluhu jijini Tanga dhidi ya wenyeji wao Coastal Union.
Mabao mawili ya Hamis Kiiza kila moja katika kipindi na jingine la Frank Dumayo yalitosha kuwapa nafuu vijana na Ernie Brandts ambao Jumapili walishindwa kulinda ushindi wao wa mabao 3-0 na kulazimishwa sare ya mabao 3-3 na watani zao Simba.
Kiiza akifunga bao la kwanza dakika ya 12 kwa krosi safi ya Simon Msuvah, goli lililodumu hadi kipindi cha kwanza kilipoisha.
Kipindi cha pili Yanga ilionekana kuzidisha mashambulizi dhidi ya wageni hao wa Ligi Kuu na kuongeza bao la pili dakika ya 73 kupitia Frank Domayo kabla ya Kiiza kurudi tena nyavuni dakika ya 81 na kuipa Yanga pointi tatu muhimu zilizowafanya wafikishe pointi 19.
Hata hivyo ushindi huo haukuisaidia Yanga kutoka nafasi ya nne kwani watani zao Simba waliongeza pointi moja wakiwa uwanja wa Mkwakwani Tanga baada ya kutoka suluhu na Coastal Union na kufikisha pointi 20 zilizowarejesha kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo.
Simba imelingana pointi na Azam na Mbeya City, lakini Wekundu wa Msimbazi wana uwiano mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa na hivyo kurejea katika uongozi ikisubiri pambano lake la Jumapili dhidi ya Azam kwenye mfululizo wa ligi hiyo.
Katika pambano la Yanga na Rhino Brandts alipangua kikosi chake kwa kumpanga kipa Deo Munishi Dida, huku Ally Mustafa Barthez, Athumani Chuji na Nadir Cannavaro wakiwa nje ya dimba.

No comments:

Post a Comment