NAIBU Waziri wa Mawasiliano Sayansi na Teknolojia, Mh. January Makamba
anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika hafla ya utoaji wa tuzo kwa mwana
soka bora wa mwaka katika ligi kuu ya Vodacom mwaka 2013, itakayofanyika
katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.
Tuzo
hiyo itashuhudia wachezaji walioingia hatua ya Tano bora, AMRI KIEMBA,
HARUNA NIYONZIMA, SHOMARI KAPOMBE, THEMI FELIX, na KELVIN YONDANI
wakichuana kuwania umwamba wa soka Tanzania, Baada ya kupigiwa kura na
mashabiki na Kamati maalum chini ya Mwenyekiti wake Zamoyoni Mogela
kuchambua majina hayo kulingana na kura walizopata.
Akizungumza juu ya hafla hiyo, Mkuu wa
Kitengo cha Masoko na Mawasiliano Kelvin Twissa amesema, wanafurahi kuwa
sehemu ya maendeleo ya soka nchini na siku zote kampuni yake imekuwa
msitari wa mbele katika kuunga mkono michezo nchini, hususani mchezo wa
soka na kuhakikisha unakuwa moja ya ajira muhimu kwa watanzania.
“Vodacom tumeendelea kuwa wadau muhimu
katika mapinduzi ya soka la Tanzania, sasa mpira umekuwa zaidi ya
burudani kwa watanzania kutokana na chachu ambayo tumeiweka tangu tuanze
kudhamini ligi kuu, ambayo sasa imekuwa na ushindani mkubwa na thamani
yake inazididi kupanda siku hadi siku,” alisema Twissa.
Aidha Twissa amesema kampuni yake
itaendelea kushirikiana na wadau wengine wote wanaopenda maendeleo ya
soka bila kusita kutokana na namna ambavyo kampuni yake imejidhatiti
katika kuinua michezo nchini.
“Mafanikio yanayopatikana katika soka
letu sasa hayajapatikana hivivi ni kutokana na dhamira tuliyoiweka
katika kuinua mchezo huu wa soka na uwekezaji mkubwa tulioufanya hadi
sasa, watu ambao wanaleta mafanikio haya ni wachezaji ambao wamekuwa
wanapambana kufa na kupona kutoa burudani kwa Watanzania, Ni lazima
tuwaenzi wachezaji hawa kwa njia tofauti tofauti,” alisema Twissa.
Kwa upande wake Meneja Masoko wa MCL
Bernad Mukasa amesema kuwa, wamefurahi kushirikiana na Naibu waziri Mh.
Makamba katika utoaji wa tuzo hizi, ambazo zinatambua mchango wa
wanasoka nchini.
“Tuzo hizi zinatambulika rasmi kwa jina la zitaitwa MWANASPOTI
BORA WA SOKA WA VODACOM 2013. Ni za kipekee na za kwanza kabisa nchini
kwa wigo wa wachezaji wanaohusishwa, ushirikishwaji wa uteuzi wa
mshindi, na vigezo husika.” alisema Mukasa na kuongeza.
“Kwa mwaka huu, licha ya kumpata
Mwanaspoti Bora wa soka wa mwaka , pia tutatoa Tuzo kwa “categories”
zaidi ya 10 ikiwemo kocha bora, mwamuzi bora, mchezaji bora wa kike,
mchezaji bora chipukizi, “1st eleven”, goli bora, mchezaji
bora wa kigeni, Mchezi bora wa kulipwa anayecheza nje, na Kipengele
kingine kitajulikana siku ya ijumaa,” alisema Mukasa.
Mukasa alihitimisha kwa kutoa wito kwa
Watanzania kuendelea kuwapigia kura wachezaji hao kwa kuandika ujumbe
mfupi unaoanza na neno KURA kisha jina la mchezaji anayemchagua kati ya
hao waliotajwa na kisha kutuma kwenda namba 15678.
No comments:
Post a Comment