Mwenyekiti wa Simba aliyetimuliwa Ismail Rage |
King Kibadeni |
KAMATI ya Utendaji ya Klabu ya Simba imefanya mapinduzi yenye utata baada jana kutangaza kumsimamisha kwa muda usiojulikana Mwenyekiti wao, Ismail Aden Rage, lakini uamuzi huo ukionekana kwenda kinyume na Kununi za Shirikisho la Soka nchini, TFF.
Kamati hiyo pia imeamua kuwatimua Kocha Mkuu, Abdallah Kibaden "King" na msaidizi wake Jamhuri Kihwelu 'Julio' na kumtangaza Kocha mpya kwamba atakuwa ni raia wa Croatia, Zdravok Logarusic ambaye atasaidiwa na nahodha wa zamani wa timu hiyo ambaye kwa sasa anainoa Simba B, Selemani Matola.
Katiba ya TFF
Hata hivyo, Katiba ya TFF ambayo ndiyo Katiba mama inayopaswa kufuatwa na vyama vya soka na klabu zote zilizo chini ya shirikisho hilo lenye mamlaka ya juu kisoka nchini, hairuhusu mapinduzi na wajumbe wote wa kamati za utendaji wa kuchaguliwa wanatakiwa wakae madarakani kwa muda wa miaka minne.
Ibara ya 31 (6) cha Katiba hiyo kinaeleza kwa tafsiri isiyo rasmi; "Mjumbe wa kamati ya utendaji anaweza kuondolewa baada ya yeye mwenyewe kuandika barua ya kujiondoa, kutohudhuria vikao vinne mfululizo vya kamati ya utendaji, kushindwa kufanya kazi za kamati ya utendaji kutokana na kuugua hadi kufikia hatua ya mgonjwa mahututi ndani ya kipindi cha miezi 12 na kupatikana na hatia ya kutenda kosa la jinai au kufungwa pasi na dhamana."
Kusimamishwa kwa Rage kumetokea ikiwa ni siku mbili tu baada ya kiongozi huyo kukamilisha usajili wa wachezaji wawili wapya, kiungo Awadh Juma kutoka kwa mabingwa wa Tanzania Bara 1999 na 2000, Klabu ya Mtibwa ya Morogoro na mshambuliaji Ally Badru akitokea Klabu ya Canal Suez ya Ligi Kuu ya Misri.
Akizungumza jana kwenye makao makuu ya klabu hiyo yaliyopo mtaa wa Msimbazi, Kariakoo jijini Dar es Salaam, aliyekuwa Kaimu Makamu Mwenyekiti, Joseph Itang'are 'Kinesi', alisema kamati ya utendaji imemteua yeye kukaimu nafasi ya mwenyekiti.
Itang'are alisema kikao cha kamati hiyo kilichokutana juzi usiku kilifikia uamuzi huo kutokana na kutokuwa na imani na Rage na kueleza kwamba amekuwa akifanya maamuzi mbalimbali binafsi bila ya kushirikisha kamati.
Alisema maamuzi waliyofanya ni kwa mujibu wa ibara ya 30 (m) ya Katiba ya Simba na yametokana na sababu mbili, mojawapo ikiwa ni kitendo cha Rage kutangaza kuahirisha mkutano wa marekebisho ya katiba ya klabu hiyo kama walivyowaeleza wanachama kwenye mkutano mkuu uliopita.
"Mwenyekiti amekiuka masuala mbalimbali na maamuzi tuliyofanya ni sahihi kwa sababu tunataka Simba iende mbele, isirudi nyuma...ni kwa nia nzuri yenye lengo la kuboresha na siyo kumkomoa tu, wajumbe wote wa kuchaguliwa tulihudhuria akiwamo Hanspope (Zacharia) ambaye ni mjumbe wa kuteuliwa," alisema Itang'are.
Alieleza kuwa, kocha huyo mpya anatarajiwa kuwasili hapa nchini Desemba Mosi, mwaka huu na siku inayofuata ataanza kazi rasmi kwa ajili ya kuiandaa timu na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara utakaoanza Januari 25 mwakani.
Aliongeza kuwa, kamati hiyo itaitisha mkutano mkuu wa marekebisho ya katiba ifikapo Desemba Mosi ambao pia utajadili hatma ya mwenyekiti huyo waliyemsimamisha.
Akitangaza uamuzi huo, Itang'are alifuatana na wajumbe wenzake wa kamati ya utendaji ambao ni pamoja na Swedy Mkwabi, Ibrahim Masoud 'Maestro', Francis Waya, Saleh Pamba, Daniel Manembe, na Katibu Mkuu, Evodius Mtawala.
Rage hakupatikana katika simu yake ya mkononi kueleza maamuzi hayo ya kamati ya utendaji ambayo ilikutana siku moja baada ya yeye kusafiri.
TFF: Tunasubiri barua Rage kusimamishwa
TFF imesema itatoa ufafanuzi kuhusu kusimamishwa kwa Rage baada ya kupata barua rasmi kutoka kwa uongozi wa klabu hiyo kongwe nchini.
Akizungumza na NIPASHE jijini Dar es Salaam jana, Kaimu Katibu Mkuu wa TFF, Boniface Wambura alisema bado hawajapata barua kutoka kwa uongozi wa Simba kuhusu kusimamishwa kwa kiongozi huyo.
"Kwa sasa hatuwezi kuzungumzia suala hilo kwa sababu bado hatujapata barua rasmi kutoka kwa uongozi wa Simba juu ya kumsimamisha mwenyekiti wao (Rage). Tutatoa ufafanuzi baada ya kupata taarifa rasmi," alisema Wambura.
Kumbuka
Ikumbukwe kuwa Kinesi alichaguliwa kama mjumbe tu wa kamati ya utendaji na makamu mwenyekiti ni nafasi ambayo anakaimu baada ya kujiuzulu kwa Geoffrey Nyange ‘Kaburu’.
Kwa mantiki hiyo, Simba kwa sasa inaongozwa bila kuwapo kwa kiongozi mkuu wa kuchaguliwa kwani tayari aliyekuwa Makamu Mwenyekiti, ‘Kaburu’ naye alijiuzulu na nafasi yake inashikiliwa na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Kinesi ambaye kwa sasa anaishikilia tena hiyo ya mwenyekiti.
Kibadeni alonga
Alipotafutwa na NIPASHE jijini Dar es Salaam jana mchana, Kibadeni alisema hana pingamizi na uamuzi uliyofanywa na uongozi wa Simba dhidi yake na kwamba anasubiri barua rasmi juu ya kutimuliwa kwake.
"Mpaka sasa (saa 6:47 mchana) bado sijapata barua ya kusimamishwa kwangu kuifundisha Simba, lakini sina pingamizi lolote na uamuzi huo. Naamini nitalipwa haki yangu kulingana na makubalino yetu yaliyomo kwenye mkataba wangu na klabu," alisema Kibadeni.
"Nitaeleza zaidi kuhusu suala hili baada ya kupata barua rasmi ya kusitishwa kwa mkataba wangu na Simba," alifafanua zaidi Kibadeni, ambaye alianza kukinoa kikosi cha Simba msimu huu akitokea Klabu ya Kagera Sugar, akichukua mikoba ya Mfaransa Patrick Liewig, ambaye pia uongozi wa Simba ulisitisha mkataba naye baada ya timu yao kumaliza nafasi ya tatu katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu uliopita.
Julio hakupatikana jana kuzungumzia suala hilo. Klabu ya Simba imekuwa na utaratibu wa kutimua makocha kila msimu, na wakati mwingine katikati ya msimu. Kutimuliwa kwa Kibadeni kunaifanya klabu hiyo kufikisha idadi ya makocha wakuu watatu waliotimuliwa ndani ya misimu miwili wakianza na Mserbia Milovan Cirkovic kabla ya Mfaransa Liewig.
NIPASHE
No comments:
Post a Comment