Swagger katika pozi |
Akizungumza na MICHARAZO, Swagger alisema kipindi hicho kitakachokuwa kikionyesha tukio kali la wiki, onyesho 'live' la burudani jukwaani, mahojiano ya msanii mkali wa wiki pamoja na kuangalia watoto wa mitaani waishivyo na pamojana mapitio ya filamu, kimeshakamilika ingawa bado hajajua kitarushwa kwenye kituo gani.
"Kila kitu kimekamilika na tayari nipo kwenye mazungumzo na baadhi ya vituo vya televisheni kwa ajili ya kuruhusu kurushwa hewani, hivyo wapenzi wa burudani wakae mkao wa kula kupata burudani ya aina yake kwani Bongo Series Extra imeshiba vya kutosha," alisema.
Swagger aliyeanza kuigiza michezo ya kwenye runinga kupitia kundi la Niger Theare akiwa na mmoja wa waasisi wa michezo ya kwenye televisheni kupitia kituo cha DTV, Qudrat Olomoda 'Chombeza', alisema aliamua kuja na kipindi hicho chenye mambo mseto ili kuwakamata mashabiki ambao walikuwa wanakosa kipindi cha namna hiyo.
Alisema ukiondoa masuala ya muziki na filamu pia kipindi hicho kitakuwa kinamulika maisha halisi ya watoto wa mitaani ili kusaidia kuizundua jamii na serikali kwa ujumla kujua tatizo hilo namna lilivyo na kuangalia jinsi ya kuwasaidia.
"Hakuna asiyejua tatizo la watoto wa mitaani au wanaoishi katika mazingira magumu, lakini nani anayejua ugumu wanaokutana nao mitaani, watasaidiwaje ili kuwafanya wafurahie maisha kama watoto wengine. Hivyo tumeona tuje namna hiyo," alisema Swagger.
Swagger ambaye kwa sasa yupo mbioni kukamilisha filamu yake mpya iitwayo 'Nyaraka' iliyowashirikisha wasanii mbalimbali wakiwemo Mzee Magari na wengine alisema anatarajia maombi yake ya kurusha kipindi hicho yakikamilika na kukubaliwa mashabiki wa burudani na jamii nzima itaburudika vya kutosha.
No comments:
Post a Comment