STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, December 2, 2013

Wanawake wawili wanaswa na 'Unga' uwanja wa KIA

Kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro, Robert Boaz
Jeshi la Polisi  Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (Kia), linawashikilia wanawake wawili ambao ni wafanyabiashara wa kigeni kwa tuhuma za kukutwa wakisafirisha kilo 12.7 za dawa za kulevya maarufu kama 'unga'.

Hilo ni tukio la pili katika muda usiozidi siku saba kwa raia wa kigeni kukamatwa na dawa hizo katika uwanja huo, ikiwa ni wiki mbili  tangu Waziri wa Uchukuzi, Dk.

Harrison Mwakyembe, atishie kuwafukuza kazi maofisa wa idara za usalama watakaobainika kujihusisha na biashara hiyo  kupitishwa katika uwanja huo.

Watuhumiwa hao waliokamatwa ni jana alfajiri katika uwanja huo ni Josiane Dede Creppy (25), raia wa Togo na Grace Teta (34), raia wa Liberia ambao kwa nyakati tofauti, mmoja akijiandaa kuelekea jijini Accra, Ghana na mwingine nchini Afrika Kusini.

Kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro, Robert Boaz, aliiambia NIPASHE jana kwamba mtuhumiwa  Grace alikamatwa akiwa na kilo 10.5 za dawa hizo wakati  akisafiri kwa ndege ya Shirika la Precision Air kutoka KIA kwenda Captown nchini Afrika Kusini kupitia Nairobi, Kenya.

“Huyu alikamatwa na unga unaoaminika kuwa ni dawa za kulevya alfajiri ya saa 10:45 akitumia hati ya kusafiria yenye namba 1039080 ikimuonyesha ni mfanyabiashara na raia wa Liberia. Josiane    alikamatwa saa 8:50 alfajiri akiwa na kilo 2.2 za dawa hiyo akiwa anataka kuondoka na ndege ya Shirika la Ethiopia kelekea Ghana,” alisema Kamanda Boaz.

Hata hivyo, alisema hadi sasa Polisi hawajatambua thamani halisi ya dawa hizo na aina ya dawa hizo kwa kuwa kazi hiyo iko chini ya Mkuu wa Kitengo cha Kupambana na Dawa za Kulevya cha Jeshi la Polisi ambaye anazipeleka kwke kwa ajili ya uthamini.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kitengo cha Kuzuia Dawa za Kulevya, Kamishna Mwandamizi, Godfrey Nzowa, alisema polisi wanazifanyia uchunguzi dawa hizo ili kubaini aina yake na thamani halisi.

“Tunazifanyia uchunguzi hata zile zilizokamatwa hivi karibuni nazo bado tunazichunguza ili tujue ni aina gani, baada ya hapo tutawapa taarifa iliyokamilika,” alisema.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, raia wa Nigeria, Chubuzo John alikamatwa na kilo nne za dawa hizokatika uwanja huo,  wakati akitaka
kuondoka kwa ndege ya Shirika la Ethiopia kuelekea Roma nchini Italia.

Polisi imeahidi kumfikisha mtuhumiwa huyo mahakamani leo baada ya kupata jalada la mashtaka kutoka kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Akiwa Kia katika ziara ya kushtukiza wiki mbili zilizopita, Dk. Mwakyembe aliwaonya maofisa wa idara za usalama pamoja na maofisa wengine uwanjani hapo, kutougeuza uwanja  huo kuwa uchochoro wa kupitisha dawa za kulevya huku akitishia kuwafukuza kazi maofisa uhamiaji watakaobainika kujihusisha na biashara hiyo haramu.

CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment