TIMU ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) itacheza mechi ya kirafiki dhidi
ya Namibia (Brave Warriors) ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya michuano
ya kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Afrika (AFCON) zitakazochezwa
mwakani nchini Morocco.
Stars na Brave Warriors zitacheza mechi hiyo Machi 5 mwaka huu jijini
Windhoek, Namibia. Mechi hiyo ipo katika kalenda ya mechi za kirafiki za
Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).
Makubaliano ya kucheza mechi hiyo yamefikiwa kutokana na mazungumzo kati
ya Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi
na Rais wa Chama cha Mpira wa Miguu Namibia (NFA), John Muinjo.
Benchi la Ufundi la Brave Warriors linaongozwa na kocha mzawa Ricardo
Mannetti, na mechi hiyo itachezwa ama Uwanja wa Sam Nujoma au Uwanja wa
Uhuru jijini Windhoek.
Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager inafundishwa na
kocha Kim Poulsen kutoka Denmark na inatarajia kuanza kucheza mechi za
mchujo za AFCON Septemba mwaka huu.
Boniface Wambura Mgoyo
Ofisa Habari na Mawasiliano
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
No comments:
Post a Comment