* Ndege iliserereka na kuingia vichakani
Waziri Abubakar Khamis Bakar aliyenusurika kifo katika ajali ya ndege jana Zanzibar |
Na Suleiman Rashid Omar Pemba
WAZIRI wa Katiba na Sheria Zanzibar, Abubakari Khamis Bakari, pamoja na abiria 17 wamenusurika kifo, baada ya ndege ya shirika la ndege la ‘Zan air’ waliyokuwa wanasafiria kupata matatizo ya breki na kusererekea vichakani.
Ndege hiyo iliyokuwa na marubani wawili, iliserereka wakati inatua katika uwanja wa ndege wa Karume kisiwani Pemba ikitokea Unguja juzi jioni.
Kamanda wa Polisi Mkoa Kusini Pemba, Swalehe Mohamed Swaleh, akizungumzia ajali hiyo alisema ilitokea baada ya ndege hiyo kuwasili Pemba ikitokea Unguja.
Alieleza kuwa ilikwenda kwa kasi kama kawaida ikitarajiwa kuwa ingepunguza mwendo lakini ilishindwa kufanya hivyo.
“Ni kweli ndege hiyo ya ‘Zan Air’ ilipata hitilafu na kuingia majanini lakini abiria wote waliokuwamo na marubani wawili, walitoka salama,’’alifafanua.
Alisema polisi imeliimarisha ulinzi wa ndege na abiria hao na haikuruhusiwa watu wasiohusika kuzengea eneo hilo.
Baadhi ya mashuhuda walioishuhudia ndege hiyo walisema ilikwenda kwa kasi kubwa kama gari zinazofukuzana na kumfanya muongoza ndege uwanjani hapo kukaa pembeni akishangazwa na kilichotokea.
Walisema baada ya kuiona ikiwa haipunguzi mwendo kasi kama inavyotakiwa, ghafla iliingia majanini na kuacha barabara ya ndege.
Mkuu wa kikosi cha zima moto na uokozi kisiwani Pemba Shaban Zidi Heri Juma, alishuhudia ndege hiyo ikikimbia kwa kasi kubwa ambapo gari la zima moto liliifuata kwa haraka hadi iliposimama kichakani.
Meneja wa uwanja huo, Rajabu Ali Mussa, alisema tukio hilo lilitokea saa 10:30 jioni jana na kwamba ilipata hitilafu baada ya uchunguuzi wa awali kuonyesha matatizo ya breki.
Alifafanua kuwa wataalamu watachunguza ili kujua chanzo cha hitilafu kwenye breki.
NIPASHE
No comments:
Post a Comment