Simba itavuna nini kwa JKT Ruvu? |
JKT Ruvu itaendelea kuwa urojo kesho katika ligi kuu mbele ya Simba? |
Azam watahimili vishindo vya Prisons baada ya kung'oka Kombe la Shirikisho Afrika? |
Prisons wataendeleza ubabe wao walioonyesha kwenye mechi za duru la pili kesho kwa Azam au...?! |
Mechi hizo mbili zitachezwa kesho jijini Dar es Salaam zikiwa ndiyo pekee katika mfululizo wa Ligi Kuu Tanzania bara kukamilisha mzunguko wa 19.
Azam wanaorejea kwenye ligi baada ya kung'olewa kwenye Kombe la Shirikisho la Ferroviario de Beira wataivaa Prisons kwenye uwanja wa Chamazi, nje kidogo ya jiji, huku Simba itaikaribisha Ruvu inayonolewa kwa sasa na kocha Fred Minziro kwenye uwanja wa Taifa.
JKT walikuwa wahanga wa Prisons kwa kukubali kipigo cha 6-0 na kuweka rekodi ya kufungwa mabao nande katika mechi mbili zilizopita, kipigo kingine walipewa na ndugu zao Ruvu Shooting ambayo leo imekumbana na dhahama kwa kulazwa mabao 7-0 na watetezi Yanga.
Mechi hizo zinasubiriwa kwa hamu kwa sababu ndizo zinazoweza kubadilisha msimamo wa ligi hiyo kwa timu zilizopo kwenye Nne Bora, kwani Azam ikishinda itarejea kwenye nafasi yake ya kwanza ambayo imechukuliwa na Yanga jioni ya leo baada ya ushindi wake dhidi ya Ruvu.
Simba nayo ikishinda itaiengua Mbeya City na kukalia nafasi ya tatu baada ya vijana hao wa Juma Mwambusi kuchezea kipigo toka kwa Coastal Union jijini Tanga jioni ya leo.
Simba ina pointi 32, tatu nyuma ya Mbeya City, lakini ikiwa na uwiano mzuri ya mabao ya kufunga na kufungwa.
Azam wenyewe wana pointi 36, mbili zaidi ya Yanga wanaoongoza sasa kwa pointi 38, hali inayofanya mechi za kesho kuwa na msisimko mkubwa mashabiki wakitaka kuona Prisons itaendeleza rekodi yake ya kukusanya pointi 10 katika mechi zake nne za duru la pili na kuvunja mwiko wa Azam kupoteza mchezo!
Wana Lambalamba ndiyo timu pekee ambayo haijapoteza mechi yoyote katika ligi ya msimu huu na katika mechi zake za duru la pili imekuwa ikigawa dozi nene hali inayoifanya Prisons kuwavaa wapinzani wao hao kwa tahadhari kubwa.
Tayari timu zote nne zimekuwa zikitambiana kila moja ikidai imejiandaa kushinda, lakini matokeo ya mwisho yatategemea baada ya dakika 90 kwa namna timu hizo zilivyopigana katika kuwakabili wapinzani wao.
Simba ambayo imekuwa na mwenendo mbovu tangu duru la pili lianze itataka ushindi ili kutuliza munkari wa mashabiki na wanachama wao baada ya kujikuta wakipoteza pointi saba kati ya tisa katika mechi zao tatu zilizopita ikiambulia sare mbili dhidi ya Mtibwa Sugar na Mbeya City na kulazwa na Mgambo JKT.
Msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara 2013-2014
P W D L F A GD PTS
01.Yanga 17 11 05 01 41 12 29 38
02.Azam 16 10 06 00 29 10 19 36
03.Mbeya City 19 09 08 02 24 16 08 35
04.Simba 18 08 08 02 33 16 17 32
05.Kagera Sugar 19 06 08 05 16 15 01 26
06.Coastal Union 19 05 10 04 14 09 05 25
07.Mtibwa Sugar 19 06 07 06 23 23 00 25
08.Ruvu Shooting 19 06 07 06 20 26 -06 25
09.Mgambo 19 05 05 09 12 27 -15 20
10.Prisons 17 04 07 05 15 16 -01 19
11. JKT Ruvu 18 06 01 11 13 27 -14 19
12.Oljoro 20 02 09 09 15 30 -15 15
13.Ashanti 18 03 05 10 15 30 -15 14
14.Rhino Rangers 19 02 07 10 12 23 -11 13
No comments:
Post a Comment