Baadhi ya miili ya watu waliokufa kwenye ajali iliyosababishwa na basi la Sumry |
Ndugu, jamaa na familia za marehemu wa ajali iliyosababishwa na basi la Sumry wakiwa nje ya hospitali kusubiri kutambua miili ya ndugu zao |
Ajali hiyo ilitokea juzi kwa basi la Sumry lililokuwa linatokea Kigoma kwenda Dar baada ya kuwaparamia watu waliokuwa wakitoa msaada ya mwendesha baiskeli aliyekuwa amekufa kwa kugongwa katika kijiji cha kijiji cha Utaho, wilayani Ikungi, barabara kuu ya Singida- Dodoma.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa Singida, Geofrey Kamwela, alisema siku ya tukio hilo wananchi wakiwa na askari polisi wa doria walikuwa wamekusanyika pembezoni mwa barabara kuupakia mwili wa mwendesha baiskeli, Gerald Zefania, aliyegongwa na lori na kufa papo hapo siku hiyo saa 1:30 jioni.
Alisema wakati wakiupakia mwili huo kwenye gari la polisi namba PT 1424 huku likiwa limeegeshwa pembeni mwa barabara, basi hilo lilitokea ghafla kwa kasi na kuwagonga watu 15 na kufariki dunia papo hapo, wengine wanne walikata roho wakati wakipelekwa hospitalini.
Kamanda Kamwela alisema dereva wa basi hilo, Paulo Njilo, mkazi wa jijini Dar es Salaam baada ya kukaribia eneo hilo aliliona gari la polisi likiwa limeegeshwa pembeni kushoto mwa barabara, lakini wakati akijaribu kulikwepa ndipo alipoliparamia kundi la watu waliokuwa na askari.
Aidha, alisema dereva wa basi hilo baada ya ajali hiyo aliendelea na mwendo hadi aliposimama kilomita 25 katika makao makuu ya Wilaya ya Ikungi na kutokomea kusikojulikana, lakini juhudi za kumtafuta zinaendelea.
Kamanda huyo aliwataja askari waliokufa kuwa ni F.849 D/CPL Boniface Magubika wa CID Wilaya ya Singida, F.6837 Pc Jumanne Mwakihaba wa FFU Singida, G.7993 Pc, Novatus Tarimo wa ofisi ya RCO na G.8948 Pc, Michael Mwakihaba wa FFU Singida.
Wengine ni Ofisa Mtendaji Kijiji cha Utaho, Ramadhan Mjengi; Mwenyekiti wa Kijiji Utaho, Paul Hamis; Mwenyekiti wa Kitongoji cha Utaho, Ernest Salanga; Said Rajab, Usirika Itambu, Chima Mughenyi, Salim Juma, Abeid Ramadhan, Mwinyi Hamis na Issa Hussein, wote wakazi wa kijiji cha Utaho.
Kamanda Kamwela alisema miili ya marehemu wengine wanne bado haijatambuliwa na ndugu zao na imehifadhiwa kwenye chumba cha maiti katika Hospitali ya Mkoa wa Singida.
Kamanda Kamwela alisema majeruhi wawili kati ya nane wa ajali hiyo wamelazwa katika Hospitali ya Mkoa Singida na wengine sita wapo hospitali ya Misheni Malikia wa Ulimwengu iliyopo Puma.
Aliongeza kuwa miili ya askari polisi inatarajiwa kusafirishwa kwenda katika mikoa wanakotoka wakati wowote baada ya taratibu za kipolisi kukamilika ikiwamo kuwasiliana na ndugu zao walioko mikoa ya Kilimanjaro, Pwani, Mbeya na Iringa.