WAZIRI Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye (pichani), amenusurika kifo hivi karibuni
baada ya ndege ya shirika la Precision Air, iliyokuwa ikitoka Mwanza
kwenda Dar es Salaam kupata hitilafu ya injini.
Ndege hiyo, ambayo iliondoka Mwanza saa 2:30 usiku, ilipata hitilafu
ya injini moja muda mfupi tu baada ya kuruka, hali iliyomlazimu rubani
wa ndege hiyo kubadili mwelekeo na kutua katika Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).
Akizungumza na Mtanzania jana, Sumaye, ambaye alikuwa mmoja
wa abiria waliokuwemo kwenye ndege hiyo, alithibitisha kutokea kwa ajali
hiyo.
Sumaye alisema kitendo cha injini kupata hitilafu, ilimlazimu rubani
wa ndege hiyo kuruka na injini moja mpaka KIA, ambako walitafutiwa ndege
nyingine ili kuendelea na safari.
Alisema kutokana na tatizo hilo, abiria walilazimika kuondoka KIA kwa
kugawanywa kwenye ndege tofauti zilizokuwa zikielekea Dar es Salaam
ambapo Sumaye aliondoka saa 7 kasoro usiku.
Msemaji wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Bestina
Magutu, alipotafutwa ili kujua kilichotokea kwenye ndege
hiyo, alisema kuwa hakuwa na taarifa zozote za hitilafu ya ndege hiyo.
“Hebu ongea nao wenyewe, sijapata taarifa zozote mpaka sasa, nimetoka ofisini jana sikuwa na taarifa,” alisema Magutu.
Naye Mratibu wa Masoko wa Precision Air, Hilaly Mremi, alipozungumza na Mtanzania alikiri kutokea kwa hitilafu hiyo ya ndege.
“Kwa kifupi hakuna ajali iliyotokea, hitilafu zinazotokea kwenye
ndege ni za kawaida kama ambavyo gari inaweza kuharibika na kupakiwa
pembeni,” alisema Mremi.
Alisema safari za shirika hilo zinaendelea kama kawaida na kutaja namba ya ndege hiyo kuwa ni TW 415.
Ndani ya wiki hii, ndege mbili za shirika hilo zimenusurika ajali baada ya kupata hitilafu wakati zikiwa angani.
Mbali na ndege hiyo aliyokuwemo Sumaye, ndege nyingine ya shirika
hilo yenye namba ya safari Pw 77 na ya usajili TWC, iliyokuwa ikitoka
Mwanza kwenda Kilimanjaro ilinusurika kupata ajali juzi jioni na hivyo
kulazimika kurudi na kutua kwa dharura uwanjani hapo baada ya kupata
hitilafu ikiwa angani.
Mbali na Sumaye, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, naye aliwahi
pia kupata ajali mwaka jana akiwa kwenye ndege za shirika hilo.
Lowassa alikuwa miongoni mwa abiria 37 waliokuwa wamesafiri na ndege
hiyo ambayo ilipasuka magurudumu manne ilipokuwa ikitua katika Uwanja wa
Ndege wa Arusha.
Katika ndege hiyo pia kulikuwa na maofisa mbalimbali wa Serikali na
Jeshi la Wananchi, ambao walikwenda kuhudhuria sherehe ya kutolewa
kamisheni kwa maofisa wa jeshi katika Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi
Monduli (TMA).
MTANZANIA
No comments:
Post a Comment