STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Thursday, December 25, 2014

Kivumbi Ligi Kuu ya VPL kuanza kutimka tena kesho

Simba
Kagera Sugar
Ndanda Fc

Mtibwa Sugar
BAADA ya mapumziko ya karibu miezi miwili, vumbi la Ligi Kuu Tanzania Bara inatarajiwa kuanza kutimka tena kuanzia kesho kwa pambano moja litakalochezwa kwenye uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam kwa kuzikutanisha Simba na Kagera Sugar.
Simba ambayo imelitumia vyema dirisha dogo la usajili kwa kufanya usajili wa baadhi ya nyota kuimarisha kikosi chao itaivaa Kagera ikitokea Zanzibar ilipokuwa imeweka kambi yao tangu Jumapili iliyopita.
Mabingwa hao wa zamani katika dirisha dogo imewaongeza kikosini, nyota kutoka Uganda, Dan Sserunkuma na mdogo wake, Simon Sserunkuma na beki Juuko Mursheed sambamba na beki wa pembeni kutoka Mtibwa Sugar, Hassan Kessy.
Timu hiyo ambayo katika mechi saba zilizopita iliambulia ushindi mmoja tu dhidi ya Ruvu Shooting ikiwa ni baada ya miezi nane ya kucheza bila kushinda tangu msimu uliopita itakuwa na kazi nguvu mbele ya Kagera ambayo katika dirisha dogo la usajili haikusajili mchezaji yeyote na rekodi yake mbele ya Simba kila wanapokutana jijini Dar es Salaam inawabeba.
Kwa misimu miwili mfululizo timu hiyo imekuwa ikiiwekea nguvu Simba kwenye uwanja wa Taifa, jambo linalotarajiwa kutokea hata katika mchezo huo kutokana na maandalizi iliyofanya timu hiyo chini ya kocha kutoka Uganda Jackson Mayanja.
Katika msimu wa 2012-2013 timu hizo zilitoshana nguvu ya kufungana mabao 2-2 na msimu wa mwaka jana matokeo yaliishia kwa sare ya 1-1 na kuibua vurugu kubwa kutoka kwa mashabiki wa Simba waliokuwa hawajafurahishwa na bao la kusawazisha la wapinzani wao.
Katika mechi hiyo ya kesho, Simba wanaivaa Kagera wakiwa wametoka kupata ushindi katika mechi ya Nani Mtani Jembe dhidi ya Yanga na huku ile dhana kwamba kundi la wanachama maarufu kama Ukawa walikuwa wakiisababisha timu kupata sare mfululizo haipo tena.
Katika msimamo wa sasa Simba wanakamata nafasi ya saba wakiwa na pointi 9 wakati wapinzani wao wapo nafasi ya tano wakijikusanyia pointi 10 baada ya kila mmoja kucheza mechi saba.
Ligi hiyo itaendelea pia mwishoni mwa wiki kwa michezo sita tofauti, Jumamosi timu za Mtibwa Sugar na Stand United ziaonyeshana kazi kwenye uwanja wa Manungu, mjini Morogoro, Prisons-Mbeya itaikaribisha Coastal Union mjini Mbeya na  'ndugu' JKT Ruvu na Ruvu Shooting zitakwaruzana uwanja wa Chamazi, huku Jumapili Mbeya City na Ndanda Fc zitakwaruzana uwanja wa Sokoine-Mbeya, Polisi Moro kuialika Mgambo JKT kwenye uwanja wa Jamhuri-Morogoro na wawakilishi wa Tanzania kwenye michuano ya kimataifa Yanga na  Azam zitaonyeshana ubabe kwenye uwanja wa Taifa.
Mabingwa watetezi wataivaa Yanga wanaouguza majeraha ya kipigo cha mabao 2-0 cha mechi ya 'bonanza' ya Nani Mtani jembe toka kwa watani zao Simba, wakiwa wanatokea Uganda walipoenda kuweka kambi ya siku 10.

No comments:

Post a Comment