Algeria wakishangilia ushindi wao dhidi ya Bafana Bafana |
Senegal walivyokuwa wakiiadhibu Ghana katika mechi ya kundi C |
Ivory Coast na Cameroon zilizopo kundi D zitacheza mechi zao za kwanza za kukamilisha raundi ya kwanza ya makundi kwa kupepetana na Guinea na Mali katika mechi zitakazochezwa usiku wa leo katika mji wa Malabo.
Tembo wa Afrika, Ivory Coast wataanza kibarua chao mapema kwa kuumana na Guinea kabla ya Cameroon kuivaa Mali katika pambano la usiku.
Timu hizo zilizofanya vema kwenye mechi zao za kuwania kufuzu fainali hizo zitakuwa zikihitaji ushindi katika mechi zao ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kusonga mbele baada ya 'vigogo' wenzao Ghana usiku wa jana kutolewa nishai na Senegal kwa kucharazwa mabao 2-1 huku Afrika Kusini ambao walifuzu fainali hizo bila kupoteza mchezo wowote katika kundi lake lililokuwa na mabingwa watetezi Nigeria waliokwama kwenda Guinea ya Ikweta ilinyukwa mabao 3-1 katika mechi za kundi la kifo la C.
Gervinho, Wilfried Bony wanatarajiwa kuiongoza Ivory Coast katika pambano la mapema usiku, ili kuibeba timu yao ambayo iliukosa mwaka 2012 michuano hiyo ilipofanyika katika nchi ya Guinea ya Ikweta iliyoshirikiana na Gabon kuziandaa fainali hizo zilizotwaliwa taji na Chipolopolo ya Zambia.
Mpaka sasa raundi ya kwanza ya makundi ikitarajiwa kukamilisha leo, ni timu tatu tu zilizoweza kupata ushindi katika mechi zao za awali, wakiwamo Gabon waliowatoa nishai Burkina Faso katika mechi za kundi A ambazo zitashuka tena dimbani kesho kwa mechi za pili ambapo wenyeji waliolazimishwa sare tya 1-1 na Jamhuri ya Kongo watavaana na Burkina Faso na vinara wa kundi hilo Gabon itaumana na Kongo.
No comments:
Post a Comment