STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Sunday, January 18, 2015

MTIBWA, JKT RUVU NANI KUIENGUA AZAM?

JKT Ruvu
Mtubwa Sugar
BAADA ya mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Azam kukalia kiti cha uongozi kwa kuiengua Mtibwa Sugar iliyokuwa imeking'ang'ania tangu ligi ianze kufuatia ushindi wake wa bao 1-0 ugenini dhidi ya Stand Utd, Wakata Miwa wa Manungu watajiuliza mbele ya maafande wa JKT Ruvu.
Timu hizo mbili zinatarajiwa kuumana jioni ya leo kwenye moja ya mechi mbili zinazochezwa leo kwenye mfululizo wa ligi hiyo, pambano litakalochezwa uwanja wa Chamazi, huku pambano jingine likiwa ni kati ya Wagosi wa Kaya, Coastal Union dhidi ya Polisi Moro mchezo utakaopigwa uwanja wa Mkwakwani-Tanga.
Mtibwa walifungwa na Simba kwa mikwaju ya penati 5-4 katika pambano la fainali ya Kombe la Mapinduzi na kuwa kipigo cha kwanza katika mechi za mashindano kwa msimu huu, na mchezo wa leo utakuwa na jasho na damu ili kurejea kileleni au kuwapisha maafande hao kukwea kileleni kwani wanalingana nao pointi.
JKT wapo nafasi ya tatu kwenye msimamo wakilingana pointi na Mtibwa sote zikiwa na pointi 16 na timu yoyote itakayoibuka na ushindi itaipiku Azam wenye pointi 17 baada ya ushindi wake wa jana.
Kocha wa Mtibwa Sugar, Mecky Mexime ametamba kuwa michuano ya Mapinduzi imewaivisha vema, licha ya kwamba hakufanikiwa kuitwaa ubingwa kama dhamira yao ilivyokuwa.
"Tunarejea kwenye ligi tukiwa tumekamilika, tuna hasira na dhamira ya kuendelea kulinda rekodi yetu ya kutopoteza mchezo wowote katika ligi hiyo," alisema Mexime.
Naye kocha wa timu ya JKT, Fred Felix Minziro alisema kuwa ameandaa vijana wake kuhakikisha wanaendelea vipigo kwa wapinzani wake ndani ya Ligi Kuu ili kutimiza lengo la kuiweka timu hiyo katika nafasi nzuri zaidi.
"Vijana wangu wapo tayari kwa vita, tunachotaka ni kupata ushindi bila kujali tunacheza na timu ipi," alisema Minziro.
Katika mechi nyingine za ligi hiyo zilizochezwa jana, Simba ikilata ushindi wa mabao 2-0 dhidi Ndanda mjini Mtwara, Yanga iling'anga'niwa na Ruvu Shooting kwa kutofungana kama ilivyokuwa kwa Mgambo JKT dhidi ya Prisons Mbeya na Kagera Sugar ililala nyumbani kwa bao 1-0 toka kwa Mbeya City.

No comments:

Post a Comment