STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Sunday, March 1, 2015

CHELSEA, SPURS KATIKA FAINALI YA KISASI

KLABU za Chelsea na Tottenham Hotspur zinatarajiwa kuvaana leo katika pambano la kisasi la fainali za Kombe la Ligi (Capital One).
Pambano hilo litakalochezwa kwenye uwanja wa Wembley linarejesha mchezo wa fainali za mwaka 2008 ilizozikutanisha timu hizo kwenye uwanja huo na Spurs kuitambia Chelsea kwa mabao 2-1.
Katika pambano hilo lililochezwa Februari 24, 2008, Spurs ilinyakua taji hilo katika muda wa nyongeza baada ya dakika 90 kumalizika kwa timu hizo kufungana bao 1-1 Chelsea wakitangulia kabla ya Spurs kurejesha.
Kadhalika pambano hilo la Fainali hizo za Kombe la Ligi limekuja ikiwa ni wiki kadhaa tangu Spurs walipoitoa nishai Chelsea kwa kuichapa mabao 5-3 katika pambano la marudiano ya Ligi Kuu ya England.
Awali Spurs ilicharazwa mabao 3-0 nyumbani kwa Chelsea mwaka uliopita na waliporudiana White Hart Lane waliwashughulikia Chelsea jambo linalofanya mechi ya leo kujaa visasi vitupu.
Chelsea chini ya Jose Mourinho itawakosa baadhi ya nyota wake akiwamo Nimanja Matic aliyefungiwa mechi mbili baada ya kupungiwa adhabu na FA kwa kadi nyekundu aliyoipata wiki iliyopita.
Hata hivyo timu hiyo inapewa nafasi kubwa ya kuwatambia wapinzani wao ambao wanauguza machungu ya kung'olewa kwenye michuano ya Ligi Ndogo ya Ulaya (UEFA Europa League) na Fiorentina ya Italia.
Ikiwa na wakali kama Ces Fabrigas, Diego Costa, Eden Hazard, Willian na wengine, Chelsea itapenda kutwaa taji hilo ili kuweka hazina kwa msimu huu baada ya awali kutolewa katika Kombe la FA.
Vinara hao wa Ligi Kuu wanapaswa kuwa makini na kinda linalotisha Harry Kane ambaye amekuwa wakiwaliza makipa hodari kama alivyoonya kipa wa Chelsea, Thibaut Courtois.
Rekodi zinaonyesha kuwa timu hizo zimeshakutana mara 134, Chelsea ikishinda mara 57 na wapinzani wao mara 44 na mechi 33 zikiisha kwa sare na pambano la leo litakuwa la 135 kwao katika michuano yote.
Je, ni Chelsea au Spurs atakayecheka leo katika uwanja wa Wembley? Bila shaka ni suala la kusubiri kuona ila kwa hakika ni bonge la mechi.

No comments:

Post a Comment