STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Saturday, March 7, 2015

Wawili waumia Twiga Stars ikijianda kuvaana na Zambia

WACHEZAJI wawili wa timu ya Taifa ya wanawake, Twiga Stars, wameshindwa kufanya mazoezi kutokana na kuwa majeruhi kwenye Uwanja wa Karume, Ilala jijini Dar es Salaam

Wachezaji ambao ni majeruhi ni Fatuma Khatib anayecheza beki ya kulia na Ziada Ramadhani beki wa kushoto na waliumia kwenye mchezo wa kirafiki wa timu hiyo dhidi ya timu ya makipa ikiwa ni maandalizi ya mchezo wa kufuzu Kombe la Mataifa Afrika dhidi ya Zambia Machi 22, mwaka huu.

Akizungumzia hali zao kocha wa Twiga Stars, Rogasian Kaijage alisema kuwa wachezaji hao wanaendelea na matibabu na anatarajia wiki ijayo watakuwa wamepona.

“Leo hawakufanya mazoezi kwa sababu wana maumivu, lakini natarajia mapema wiki ijayo watakuwa wamepona kwani wanaendelea vizuri na matibabu”, alisema Kaijage

Kaijage alisema kutokana na program ya mazoezi aliyoendesha tangu timu hiyo ianze kambi mwishoni mwa mwezi uliopita anatarajiwa kuwa na mchezo mmoja wa kujipima nguvu katikati ya mwezi huu.

Twiga Stars ambayo imeweka kambi katika Hosteli za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) zilizopo ndani ya Uwanja wa Karume, Ilala, Dar es Salaam imeingia moja kwa moja katika hatua ya pili kucheza na Zambia kufuatia kuwa na matokeo mazuri katika msimamo wa viwango vya soka la wanawake barani Afrika.

Wachezaji waliopo kwenye kikosi cha Twiga ni Asha Rashid, Esther Chaburuma, Fatuma Bushiri, Fatuma Hassan, Fatuma Mustapha, Fatuma Omari, Eto Mlenzi, Mwajuma Abdallah, Sofia Mwasikili, Zena Khamis, Mwanahamisi Omar, Fadhila Hamad, Anastazia Anthony na Shelder Boniface.

Wengine ni Thereza Yonna, Happines Hezron, Amina Ally, Donizia Daniel, Fatuma Issa, Vumilia Maarifa, Maimuna Hamisi, Najiati Abbas, Stumai Abdallah, Zuwena Aziz, Irene Joseph, Dawa Haji Vuai, Belina Julius na Amina Ramadhani.

No comments:

Post a Comment