Juma Abdul |
Juma Abdul (12) akiwajibika kimataifa |
Beki huyo anayeichezea pia Taifa Stars ameteuliwa kuwa Mchezaji Bora wa Ligi Kuu Bara kwa mwezi Aprili akimbwaga straika wake,Ngoma na kiungo wa JKT Ruvu, Hassan Dilunga.
Katika rekodi za Bodi ya Ligi Tanzania Bara (TPLB) iliyoketi Jumamosi iliyopita, imeonesha kwamba Abdul alicheza mechi zote tano za Ligi Kuu kwa mwezi Aprili ambapo pia aliifungia timu yake bao katika harakati za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu msimu wa 2015/16.
Rekodi hizo pia zinaonyesha kwamba beki huyo hakuonyeshwa kadi hata moja katika michezo hiyo mitano sambamba na kutoa mchango mkubwa katika michezo aliyoshiriki kwa mwezi Aprili, 2016.
Beki huyo atazawadiwa fedha Sh. Milioni 1= na wadhamini wa Ligi hiyo, Kampuni ya mtandao wa simu za mkononi ya Vodacom.
Uwezo aliouonyesha Abdul ulisababisha Kocha wa Taifa Stars, Charles Boniface Mkwasa ‘Master’ kumjumuisha katika kikosi chake kwa ajili ya mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya Harambee Stars ya Kenya kadhalika Mafarao wa Misri katika mechi ya kuwania kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika utakaofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Juni 4, mwaka huu.
Wachezaji bora wa miezi minne iliyopita ni kiungo Thabani Kamusoko wa Young Africans (Desemba 2015), beki Shomari Kapombe wa Azam (Januari 2016), Mshambuliaji Mohammed Mkopi wa Prisons (Februari 2016) na Shiza Kichuya wa Mtibwa Sugar (Machi 2016).
No comments:
Post a Comment