STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, August 19, 2016

Duh! Liverpool yaukacha Uwanja wao wa Anfield mwezi mzima


LIVERPOOL iliyoanza vema Ligi Kuu ya England msimu huu kwa kuikandika Arsenal kwa mabao 4-3 inatarajia kucheza mechi zake tatu zinazofuata ikiwa ugenini kitu ambacho si cha kawaida.
Sababu inayoifanya Liverpool isicheze kwenye Uwanja wao wa Anfield kwa mwezi mzima na kucheza mechi tatu mfululizo za EPL ugenini ni kwa sasa ni kutokana na ombi lao wenyewe la kutaka uwanja wao ukarabatiwe.
Mechi inayofuata kwa Liverpool ni kesho Jumamosi ikivaana na Burnley ugenini, lakini imebainika kuwa wametaka hivyo ili kupisha kukamilika kwa ujenzi wa upanuzi wa Jukwaa Kuu la Uwanja wao wa Anfield.
Jukwaa hilo limepanuliwa na kuongezwa ngazi 3 juu za kukalia mashabiki, kupanua ukumbi wa Wachezaji kuingia na kutoka uwanjani kutoka vyumba vya Kubadili Jezi, mabenchi ya wachezaji wa akiba na Jopo lao la Ufundi kutengenezwa upya. Pia sehemu maalum kwa walemavu itatengenezwa upya sambamba na kuboreshwa kwa miundo mbinu ya watazamaji.
Jukwaa Kuu la Anfield litaongeza viti 8,500 na kuufanya Uwanja huo sasa uingize jumla ya Watazamaji 54,000.
Mechi ya kwanza kabisa kwa Liverpool kukanyaga Anfield Jijini Liverpool msimu huu itakuwa Septemba 10 watakapovaana na Mabingwa Watetezi Leicester City.

Arsene Wenger awapa moyo mashabiki Arsenal

Kocha Arsene Wenger
KWISHA habari yake. Kocha Arsene Wenger anayetajwa kama mmoja ya makocha wabahili katika kununua wachezaji, amelegea baada ya kusisitiza kuwa,  yuko tayari kutumia fedha kununua nyota wapya ndani ya Arsenal kabla Dirisha la Uhamisho halijafungwa Agosti 31.
Hadi sasa, katika kipindi hiki cha Uhamisho kilichoanza rasmi Julai Mosi, Arsenal imeshagomewa na Jamie Vardy wa Mabingwa wa England Leicester City wakati Ofa yao kumnunua Straika wa Lyon Alexandre Lacazette imegomewa na Klabu hiyo ya France na pia nia yao kumchukua Sentahafu wa Valencia ya Hispania Shkodran Mustafi imegota mwamba.
Matukio hayo yamewafanya Mashabiki wa Arsenal kuamini Wenger na klabu hawana nia kutumia Fedha ikibidi.
Akihojiwa nini kinajiri kuhusu Mustafi, Wenger alijibu: “Naamini ni bora tusizungumzie kuhusu wachezaji binafsi, lakini sisi tunafanya kazi kwa bidii. Nyie mnaamini kabisa kuwa sipo tayari kutumia Fedha lakini nakuhakikishia tupo tayari kutumia Fedha!”

Mavugo kimeeleweka, kuivaa Ndanda Taifa

Mavugo
Na Tariq Badru
UHONDO unakolea. Klabu ya Simba imepata hati ya uhamisho wa kimataifa  (ITC) za mastraika wake wawili wa kigeni, Laudit Mavugo na Frederic Blagnon.
ITC hizo zimetua leo Ijumaa mchana baada ya kukamilisha uhamisho wao na sasa wanaweza kuanza majukumu yao Msimbazi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyopostiwa kwenye mitandao na Katibu Mkuu wa Simba, Patrick Kahemele ni kwamba ITC  zimetua nchini leo mchana kutoka katika mashirikisho ya soka ya Burundi na Ivory Coast.
Blagnon Fredric Goue ametokea klabu ya Africa Sports ambao ni wapinzani wa jadi wa ASEC Mimosas ya nchini Ivory Coast.
Wakati Mavugo yeye anatokea klabu ya Vital'O ya Burundi na kupatikana kwa hati hizo kunamaliza utata wa uhamisho wa Mavugo ambaye kulitokea kwa maneno toka kwa uongozi wa klabu ya Vital’O kuwa bado ana mkataba wa mwaka mmoja jambo ambalo lilikanushwa na Mavugo.
Mavugo amewakuna mashabiki wa Simba baada yab kupiga mpira mwingi kwenye mechi ya Tamasha la Simba Day dhidi ya AFC Leopards ya Kenya na ile mechi ya URA.

Usain Bolt kashindikana Olimpiki, ashinda tena

https://ssl.gstatic.com/onebox/media/olympics/photos/o16/live/RIOEC8J0568SG_768x432.JPGKASHINDIKANA. Mwanariadha kutoka Jamaica, Usain Bolt, amedhihirisha kwamba yeye ni mwamba wa mbio za fupi baada ya kushinda Mita 200 katika michuano ya Olimpiki inayoelekea ukingoni mjini Rio de Jeneiro, Brazil.
Bolt ameshinda mbio hizo na kujinyakulia medali ya Dhahabu ikiwa ni mara ya pili baada ya kunyakua ya michuano ya Mita 100.
Bolt aliweza kushinda mbio hizo kwa urahisi kwa kutumika Sekunde 19.79 na kwa sasa anahitaji kushinda mbio za mita 400 za kupokezana vijiti ili kukamilisha medali ya tatu ya dhahabu kama alivyofanya katika michuano iliyopita.
Mapema wiki hii alidhihirisha kuwa ni mwamba wa mbio fupi pale aliposhinda mbio za mita 100 na kunyakuwa medali ya dhahabu.
Kwa upande wa Marekani imeweza kujinyakulia medali nyingine nne za Dhahabu ikiwemo ya mwanariadha wake Ashton Eaton.
Huku mkimbiaji kutokea nchini Kenya aliyekuwa ametangaza kustaafu, Ezekiel Kemboi, ameeleza kwamba ameahirisha kustaafu mara baada ya kunyang`anyway medali aliyokuwa ameshinda katika mbio za kuruka viunzi na maji.
Medali hiyo iliyochukuliwa na Mfaransa mara baada ya kukata Rufaa kwenye Mita 3000 imemfanya Kemboi kusema kuwa watakutana tena London 2017 kwenye michezo ya Olimpiki ili kuweza kudhihirisha kwamba alikuwa akistahili medali hiyo.

Pogba kuanza mambo yake Man United

KAZI imeanza. Kiungo mpya wa klabu ya Manchester United, Paul Pogba leo Ijumaa anatarajiwa kuanza kuitumikia timu yake hiyo kwa mara ya kwanza katika mchezo wa Ligi Kuu ya England dhidi ya Southampton.
Pogba aliyeondoka klabuni hapo kwa mlango wa nyuma mwaka 2012 kwenda Juventus amerejea tena Man United kwa ada ya Pauni Milioni 89 iliyovunja rekodi ya dunia, alishindwa kuanza katika mchezo uliopita dhidi ya Bournemouth.
Kilichomkwamisha nyota huyo wa Ufaransa kukipiga kwenye mchezo huo ambao Man Un ited ilishinda mabao 3-1 ni kwa sababu ya kutumikia adhabu ya mechi moja aliyotoka nayo Italia katika Ligi ya Serie A.
Akihojiwa kuhusu mchezo wa leo usiku, Pogba alisema anajisikia yuko fiti na amekuwa akifanya mazoezi kwa siku 10, lakini hata hivyo itategemea meneja wake Jose Mourinho atakavyoona inafaa.
Pogba aliendelea kudai kuwa ameshazoea hali hiyo kwani amekuwa akifanya mazoezi hata wakati alipokuwa likizo hivyo anajiona yuko sawa.
Man United itaivaa Saints ikitegemea safu yake kuongozwa na nyota wao mpya, Zlatan Ibrahimovic aliyeanza kwa makeke ndani ya klabu hiyo inayoongoza msimamo kwa uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa.

Hata hivyo mapema leo mchana Kocha Mourinho aliwahakikishia mashabiki wa Man United kuwa kiungo Paul Pogba atawavaa Southampton.
Kocha Mourinho alisema Pogba amefanya mazoezi kwa siku 11 na imekuwa rahisi kumbadili Pogba kwa vile ni kijana aliyekulia OT na anamjua kila mtu.
Alipoulizwa kama yeye anaweza kusaidia kurejesha ile hali ya timu kuiogoga Man United iliyokuwepo enzi za Sir Alex Ferguson, Mourinho alijibu: “Sio mimi. Ni timu, ndio. Na mashabiki pia. Nadhani kila kitu kinaanza hapo, uhusiano kati ya timu na mashabiki.”
Aliongeza: “Ikiwa humo Old Trafford, mashabiki wa upinzani, maelfu kadhaa wanakuwa na kelele kubwa kupita Mashabiki zaidi ya 70,000, basi sisi tupo mashakani. Inamaanisha uhusiano kati ya timu na mashabiki wake. Kukiwepo uhusiano, basi ule ukweli wa kutisha tukiwa nyumbani utarudi. Kila kitu kinaanza na uhusiano huo wa timu na mashabiki wake. Ikiwa mashabiki watahusiana na timu, wanataka nao kucheza na wakicheza, wapinzani hawana nafasi!”
Kwa taarifa yako tu ni kwamba Southampton imekuwa ikizoa pointi tatu kwenye Uwanja wa Old Trafford kwa misimu miwili sasa wakifungamana na Norwich City, Swansea City na West Bromwich Albion.


Mtamkoma! Kessy ruksa kukipiga Jangwani msimu huu

Kessy akiwajibika kwenye mechi ya Ngao ya jamii dhidi ya Azam
Na Rahma Kimwaga
YANGA inayojiandaa kupaa kwenda zao DR Congo huenda ikawa inatabasamu kwa furaha baada ya beki waliyekuwa wakimpigania kutoka Simba, Hassan Kessy kupewa uhalali wa kuanza kuitumikia timu hiyo katika Ligi Kuu Bara msimu huu.
Kessy aliyekuwa akiwekewa zengwe na Simba, licha ya ukweli ilishamaliza naye mkataba na ilionyesha wazi kutomhitaji baada ya kumfungia mechi tano za mwishoni mwa msimu uliopita kwa kitendo cha kunmchezea rafu Edward 'Rddo' Christopher aliyekuwa akiichezea Toto Africans aliyesajiliwa Kagera Sugar kwa sasa.
Kamati ya Sheria na Haki za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF)  lilipitisha jina la Kessy kuichezea Yanga sambamba na usajili wa klabu nyingine kwa msimu wa 2016-2017.
Kamati hiyo imepitisha jina la Hassan Ramadhani ‘Kesi’ kuitumikia Yanga kuanzia msimu huu 2016/17 baada ya kuona kuwa hana tatizo katika usajili badala yake madai ambayo pande husika zinaweza kudaiana wakati mchezaji anaendeleza kipaji chake.
Kamati hiyo chini ya Mwenyekiti wake, Richard Sinamtwa imepitia usajili wa timu zote na kujiridhisha kwamba suala la mchezaji Hassan Kessy limeegemea kwenye madai na si usajili ambako Simba ndiye mdai kwa kumtuhumu mchezaji huyo kuwa alianza kuitumikia Young Africans kabla ya kumaliza mkataba wake Simba SC. Mkataba wake ulifika mwisho, Juni 15, 2016.
Kama ni madai Simba inaweza kuendelea kumdai Kessy au Young Africans wakati mchezaji huyo anatumika uwanjani kwa mwajiri mpya. TFF inafuatilia na kuangalia haki ya Simba namna ya kupata haki yake baada ya kuwasilisha madai kuhusu kuvunja mkataba na mwajiri wake wa zamani.
Kanuni hazimzuii mchezaji kuendelea kucheza kwa hoja ya madai badala yake suala hilo linaweza kumalizwa wakati mashindano yanaendelea. Kamati inaendelea kupitia malalamiko na pingamizi za wachezaji wengine na inatarajiwa kutoa taarifa rasmi kuhusu wachezaji wote wakati wowote kuanzia sasa.
Katika hatua nyingine Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limezionya timu shiriki za ligi hiyo kutochezesha wachezaji wa kigeni kama hawana vibali vya kuishi, kufanya kazi na leseni inayomruhusu kucheza ligi husika kwa mujibu wa sheria za nchi na kanuni za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Vibali vya kuishi na kufanya kazi vinatolewa na Idara ya Uhamiaji Tanzania (Uhamiaji) wakati leseni ya kucheza inatolewa na TFF.
Vilevile TFF imeziagiza klabu kulipia ada za ushiriki kwa kila timu; leseni za wachezaji, ada za wachezaji na ada za mikataba.
Mchezaji hatapewa leseni ya kucheza kama uongozi wa timu hautakamilisha taratibu za malipo.
TFF pia imezikumbusha timu zinazoshiriki Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kwamba hazitapewa leseni ya mchezaji yeyote ambaye timu haikuleta mkataba wakati wa maombi ya usajili, hii ni kwa mujibu wa kanuni ya 68 vipengele vya 1, 2, 3 na 8 ya Ligi Kuu ya Tanzania toleo la 2016/2017.
Kila timu inatakiwa kuleta nakala tatu za mkataba wa mchezaji, ili kamati ya katiba, sheria na hadhi za wachezaji iweze kupitia na TFF iweze kuidhinisha mikataba hiyo. Baada ya hapo timu na mchezaji, watakuja kuchukulia mikataba hiyo hapa TFF. Ni matarajio yetu kuwa kila klabu itatimiza wajibu wake ili kuondoa migogoro kati ya timu na mchezaji na mchezaji na timu. Tunategemea kupata ushirikiano.

KUMEKUCHA VODACOM PREMIER LEAGUE 2016-2017

Mabingwa watetezi Yanga
Simba
Azam
NA RAHIM JUNIOR
MSIMU mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara maarufu kama Vodacom Premier League, VPL unatarajiwa kuanza rasmi kesho Jumamosi kwa michezo mitano, huku mtetezi Yanga ikila shushu hadi Agosti 31 kwa vile ina majukumu ya kimataifa.
Yanga inatarajiwa kuondoka siku ya Jumapili kwenda Lubumbashi nchini DR Congo kumaliza mchezo wake wa kukamilisha ratiba ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya wenyeji TP Mazembe itakayochezwa Jumanne ijayo.
Kwa mujibu wa ratiba ya VPL, kesho kuitakuwa na michezo itakayohusisha Simba ambayo itaialika Ndanda ya Mtwara kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, huku Azam itakuwa mwenyeji wa African Lyon Uwanja wa Azam Complex, Chamazi.
Mjini SHinyanga kwenye Uwanja wa Karambage, Stand United itakwaruzana na Mbao FC ya Mwanza inayoshiriki ligi hiyo kwa mara ya kwanza, wakati Mtibwa Sugar itaikaribisha Ruvu Shooting ya Pwani kwenye Uwanja wa Manungu, Turiani mjini Morogoro.
Mechi nyingine itazihusisha Maafande wa Prisons ya Mbeya itakayosafiri hadi mjini Songea, Mkoa wa Ruvuama kuvaana na wenyeji wao Majimaji kenye Uwanja wa Majimaji.
Ligi hiyo itaendelea Jumapili kwa mchezo mmoja tu,  Kagera Sugar itaialika Mbeya City kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga kabla ya Jumatano
Toto Africans haijavaana na Mwadui kwenye uwanja wa CCM Kirumba. Mechi hizo zimehamishiwa hapo kwa vile Uwanja wa Kaitaba, Bukoba bado haujakamilika kukaratabiwa na ule wa CCM Kirumba kuwa na kazi nyingine likiangushwa Tamasha la Fiesta 2016.
Ligi hiyo inaanza huku karibu timu zote zimefanya usajili wa maana na baahi kubadilisha benchi la ufundi la timu zao.
Klabu nne pekee ndizo ambazo zinashiriki ligi hiyo zikiwa na makocha wao wa msimu uliopita na zilizosalia zimebadilisha kwa kuwaleta wapya ama kubadilishana na wapinzani wao kama ilivyo kwa Mtibwa Sugar na Kagera Sugar.
Kocha Mecky Maxime aliyekuwa Mtibwa ametua Kagera Sugar na nafasi yake kuchukuliwa na Salum Mayanga aliyekuwa akiinoa Prisons Mbeya.
Makocha wengine wapya katika ligi hiyo ni Zeben Hernandez kutoka Hispania anayeinoa Azam, Joseph Omog wa Simba, Rogasian Kaijage wa Toto Africans na Etienne Ndeyirageji wa Mbao FC anayetokea Burundi.
JKT Ruvu iliyosukwa upya pia ina kocha mpya Hamis Malale 'Hamsini' aliyekuwa Ndanda wakati Ndanda sasa inanolewa na Joseph Lazaro aliyekuwa Mgambo JKT iliyoshuka daraja, huku Ruvu Shooting ikiwa na kocha mpya Seleman Mtingwe.
Africna Lyon naye inashiriki ligi hiyo baada ya kurejea kutoka Ligi Daraja la Kwanza ikiwa na kocha wa zamani wa Simba, Dragan Popadic akisaidiwa na Ramadhani Aluko, huku Majimaji Songea ikiwa chini ya Kocha Juma Mhina.
Mbali na makocha msimu huu utashuhudia vikosi vinavyoundwa na wachezaji wapya waliosajili kwenye timu hizo shiriki gumzo likiwa ni usajili wa straika kutoka Burundi, Laudit Mavugo na wakali wengine ndani ya kikosi hicho akiwamo, Shiza Kichuya, Federick Blagnon, Method Mwanjali na Mussa Ndusha.
Je, unadhani ni timu ipi itaanza msimu na mguu mzuri? Tusubiri baada ya dakika 90 za mipambano hiyo na ile ya kesho.


Ratiba ilivyo:
Kesho Jumamosi
Simba            v Ndanda
Stand Utd       v Mbao
Mtibwa Sugar v Ruvu Shooting
Azam             v African Lyon
Majimaji         v Prisons

Jumapili

Kagera Sugar v Mbeya City

Jumatano

Toto African    v Mwadui