STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Wednesday, July 7, 2010

Bileku Mpasi: Dansa na Rapa wa Empire Bakuba anayekumbukwa * Alifunika na kumtia kiwewe Papy Tax, akamuibua Kokoriko Tz *




KWA wapenzi wa muziki wanaweza kukumbuka kuwa, bendi ya Empire Bakuba ilianzishwa na watu watatu, marehemu Joseph Kabasele Yampanya 'Pepe Kalle', Papy Tex na Dilu Dilumona miaka ya 1970.
Lakini pamoja na bendi hiyo kuasisiwa na watatu hao na baadae kupewa nguvu na Jojo Ikoma, ni vigumu kutaja mafanikio yake bila kumhusisha Djouna Mumbafu 'Bikelu Mpasi' a.k.a Big One.
Bileku aliyezaliwa na kupewa majina ya wazazi wake ya Bileku Jean-Pierre Matonet, aliweza kuifanya Bakuba ie juu kinoma.
Pamoja na ukweli kuwa alichukuliwa na Pepe Kalle kama dansa na rapu wa bendi hiyo, Bileku Mpasi aliweza kupanda haraka na kuwa maarufu pengine hata waasisi wenyewe.
Kupanda kwake kwa mafanikio kulitokana na umahiri wake wa kucheza, kurapu na baadae kuimba kiasi kwamba marehemu Pepe Kalle alifikiria kumpa nafasi ya hisa zake katika bendi hiyo.
Marehemu Pepe Kalle alitokea kumpenda na kumuamini Bileku Mpasi kama alivyofanya marehemu Franco kwa marehemu Madilu Systems enzi za uhai wao walipokuwa pamoja bendi ya T.P OK Jazz.
Jitu hilo la Miraba Minne hakumpenda bure kijana huyo, bali ni kutokana na ukweli alikuwa akijituma na kuifanya Empire Bakuba iliyoanzishwa kutokana na jina la moja ya makabila ya nchini Zaire (DR Congo ya sasa) kufunika kwa sana enzi za uhai wake.
Kasi yake ya kucheza na kurapu kwa wakati mmoja ndiyo kwa sasa imekuwa ikiigwa na marapa mbalimbali wa makundi ya muziki wa Lingala kuanzia DR Congo, Congo Brazaville hadi Bongo.
Enzi zake mkali huyo alikuwa akichuana na wakali kama Robert Ekokota Wenda wa Wenge Musica BCBG kabla ya kuibuka wengine kadhaa waliofuata nyayo zao.
Wapo wengine wanaodai kuwa Bileku Mpasi ndiye muasisi wa Ma-Atalaku walioibua nchini Congo na kufanya muziki wa Lingala ama Bolingo kuchangamka mno isivyo kawaida.
Ukali wake na ushirikiano aliokuwa nao na mbilikimo Emorro na baadae Djuma Fatembo na Jully Bebe, kulimfanya Bileku kuzidi kuwa juu na hasa kwa rafu zake matata katika albamu mbalimbali.
Ingawa hakuna taarifa kamili juu ya historia kamili ya mkali huyo ambaye kwa sasa ana kundi lake binafsi la Orchestra Big One, akitamba na albamu ya Tonnerre de Brest yenye kibao cha 6600 Volts, inadaiwa alizaliwa miaka zaidi ya 40 iliyopita.
Shughuli zake za muziki alizianza katika mji wa Kalemi kabla ya kuibukia Kishansa miaka ya mwishoni ya 1970.
Mwanzoni mwa miaka ya 1980 alikuwa akifanya shughuli zake katika bendi ndogondogo kama mnenguaji kabla ya kuchukuliwa na Pepe Kalle na kuwa dansa na rapa wao.
Hata hivyo kutokana na kuonyesha kipaji kikubwa katika uimbaji, Pepe Kalle akishirikiana na mtunzi mahiri wa Empire Bakuba enzi za uhai wake, Papy Tex walimpika kuwa muimbaji mkali.
Hata hivyo ukali wake na kuwafunika wawili kati ya waasisi wa kundi hilo, inaelezwa kuwa kulimsababishia rapa huyo 'kuunda' bifu kali na Papy Tex.
Ndio maana mara baada ya kifo cha marehemu Pepe Kalle Novemba mwaka 1998, kulitokea mtafaruku kama ule wa TP OK Jazz baada ya kifo cha Franco juu ya mustakabali wa bendi hiyo na Madilu.
Ilidaiwa kuwa wanamuziki waliosalia katika bendi hiyo walikuwa na nia ya kuiendeleza Empire Bakuba, ila waasisi na waliokuwa wamiliki wake, Dilumona na Papy walianzisha zengwe baada ya kufahamika Bileku amepewa usimamizi wa hisa za Pepe Kalle.
Yeye na Gode Lufombo waliamua kujiondoa na kuiacha Bakuba mikononi mwa mwenye nayo na kwenda kujiunga na kundi la Delta Force, ambalo lilikuwepo hata kabla ya kifo cha Pepe Kalle.
Delta Force alikaa nao kwa muda tngu mwaka 1999 hadi 2002 kabla ya kuamua kujiondoa na kuwa msanii wa kujitegemea na kufanikiwa kufyatua albamu yae ya kwanza ya Tonnerre de Brest.
Albamu hiyo ilikuwa na kibao matata cha 6600 Volts, ilitolewa mwaka 2004 na kumfikisha Bileku kwenye Fainali za Tuzo za Muziki za Afrika za Kora (Kora Music Award) za mwaka huo kupitia kibao hicho, ingawa hakufanikiwa kubeba tuzo yoyote.
Miongoni mwa vibao vya albamu hiyo iliyompa mafanikio makubwa kabla ya mkali huyo kujiundia Orchestra Big One inayotamba na albamu nyingine mpya ya mwaka jana ni pamoja na 100% TVA, 6600 Volts na Cupidon Brisé.
Vibao vingine ni pamoja na Fin Du Match, Karachiga, Nez a Nez, Mihona, Onze, Respect Pepe Kalle, Tatou na Tonnerre De Brest.
Bileku anayekumbukwa na Watanzania kwa kuchangia kuibua vipaji vya madansa wa Kitanzania kama akina Kokoriko aliyeshabihiana nae, Marehemu Maxi Prest, Mrisho Mpasi na wengine ndani ya bendi yake anaimba pamoja na mdogo wa marehemu Pepe Kalle.
Mdogo huyo wa marehemu Pepe Kalle, Ally Kale amefanana mno kisauti na marehemu kaka yake kiasi ukisikiliza nyimbo za kundi hilo unaweza kudhani 'Tembo wa Afrika' amefufuka.

No comments:

Post a Comment