STRIKA
USILIKOSE
Wednesday, July 7, 2010
Sajuki: Mkali wa filamu anayeulilia mguu wa mkewe
NDOTO zake enzi akiibukia kwenye sanaa ilikuwa ni kuja kuwa mchekeshaji kutokana na kumzimia mno, msanii Athuman Amir 'King Majuto'.
Hata hivyo kupenda kwake kuangalia filamu za Sylvester Stallone 'Rambo' zilimfanya abadili upepo na kujikita kwenye uigizaji wa kawaida na kisha kujitumbukiza kwenye tasnia hiyo, ambapo leo ni mmoja wa nyota wa fani hiyo nchini.
Sajuki, ambaye majina yake kamili ni Juma Juma Issa Kilowoko, alisema hamu yake ya kufika mbali katika sanaa ya uigizaji ndiyo iliyomfanya apite kundi moja hadi jingine hadi kuangukia Kaole Sanaa, lililomtangaza vema kupitia michezo iliyokuwa ikirushwa na kituo cha runinga cha ITV.
Alisema mchezo wake wa kwanza ndani ya kundi hilo lililotoa nyota kibao wa filamu nchini ni Baragumu wa mwaka 2005 na kufuatia na michezo mingine hadi mwaka 2008 alipojitoa kundini na kujikita zaidi katika filamu, kazi yake ya kwanza ikiwa ni Revenge.
"Baada ya kupita makundi kadhaa tangu nikiwa mjini Songea nilipozaliwa, hatimaye nilitua Kaole Sanaa, lililoniivisha kabla ya kuachana nao kusaka masilahi zaidi na kujikita katika filamu," alisema.
Mbali na Revenge filamu zingine alizocheza Sajuki ni pamoja na Dhambi, Mboni Yangu, Two Brothers, Behind the Scene, Round, Shetani wa Pesa, Hero of the Church na nyinginezo.
Kwa sasa yupo mbioni kuachia kazi mbili binafsi za Vita na Briefcase zilizowashirikisha nyota kadhaa nchini akiwemo mshindi wa pili wa BBA, Mwisho Mwampamba.
Sajuki alisema fani ya filamu imemnufaisha kwa mambo mengi ikiwemo kimaisha, lakini kubwa ni kufanikiwa kumuoa mke mrembo na muigizaji mwenzake, Wastara Juma.
"Kufanikiwa kumpata Wastara na kumuoa kwangu ni jambo kubwa na la kuvutia mno kati ya mafanikio kibao niliyoyapata katika fani hii ya filamu nchini," alisema.
Mkali huyo, ambaye hupenda kucheza na watoto na shabiki wa muziki wa 'Quito', alisema kama kuna kitu kinachomkera katika sanaa hiyo ni tabia za 'Wauza Sura' wanaojiingiza kwenye skendo chafu zinazowachafua wasanii wote wa tasnia hiyo mbele ya jamii.
Alisema wasanii wenye kusaka umaarufu kwa lazima wanamnyima raha kwa vile jamii inadhani wasanii wote wana silka na tabia kama za wauza sura hao wanaojirahisi na kujidhalilisha.
Kuhusu rushwa ya ngono, Sajuki mtoto wa nne kati ya watano wa Mzee Juma Issa Kilowoko, alisema wanaojihusisha nao wanafanya hivyo kwa kujitakia kwa sababu hakuna anayelazimishwa kutoa mwili wake iwapo ana uwezo na kipaji kikubwa katika sanaa hiyo.
"Rushwa ya ngono kwa watoto wakike ni kujitakia kwa vile wana akili na ufahamu wa kujua athari za kufanya hivyo na watayarishaji wanaolazimisha hawafai na wanapaswa kuchukuliwa hatua kali za kisheria," alisema Sajuki.
Sajuki, aliyelifafanua jina lake hilo kuwa ni muunganisho wa jina la kaka yake mkubwa Salum, lake la Juma na lile la ukoo wao la Kilowoko, alisema hakuna kitu kinachomtia simanzi na kumsikitisha kama tukio la ajali ya pikipiki iliyompata akiwa na mkewe, Wastara Juma enzi wakiwa wachumba.
Nyota huyo mwenye mtoto mmoja wa kiume na anayeishukuru famili yake na Vincent Kigosi 'Ray' kwa kumfikisha hapo alipo, alisema ajali hiyo sio inayomuuma, ila kitendo cha kulazimika kuidhinisha fomu hospitalini ili Wastara akatwe mguu wake uliokuwa umeharibika kwa ajali hiyo.
"Kwa kweli kile kitendo cha kuidhinisha kukatwa kwa mguu kwa Wastara kinaniuma hadi leo, lakini sikuwa na jinsi ila kufanya hivyo ili kumuokoa," alisema Sajuki.
Hata hivyo alisema anajisikia fahari mno kuuoana na kisura huyo ambaye kwa sasa anao mguu wa bandia, kwa vile wamesaidia kuanzisha kampuni yao binafsi ya Wajey Films Production.
Mkali huyo alizaliwa miaka zaidi ya 25 iliyopita huko Songea na kusoma hadi elimu ya sekondari katika shule za Songea na Luwiko, alikoanza kuonyesha kipaji chake cha sanaa katika matamasha mbalimbali ya shule kabla ya kujitosa kwenye makundi.
Kwa sasa, Sajuki anayeitaka filamu ya Mboni Yangu kama picha kali kuliko zote alizowahi kuigiza, yupo mbioni kuachia kazi zake mbili binafsi za Vita na Briefcase zilizowashiriki wakali kadhaa na matarajio yake ni kujiendeleza zaidi ili kuleta mapinduzi katika tasnia ya filamu nchini.
.
Mwisho
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment