WAUMINI wa dini ya Kiislam na Watanzania kwa ujumla wameaswa kuchagua viongozi katika uchaguzi mkuu ujao bila kujali aina ya vyama vyao ilimradi ni watu wenye uchungu, uadilifu na dhamira ya kweli ya kuwakomboa.
Aidha waumini na watanzania wamehimiza kuhakikisha wanashiriki kwa wingi siku ya kupiga kura na kujichagulia viongozi wawatakao badala ya kusubiri kuchaguliwa kisha waje kulalama mambo yatakapokuwa yakienda kombo.
Wito huo umetolewa na Imamu wa Msikiti wa Mwenge Islamic Center, Sheikh Shaaban Mapeyo alipokuwa wakiwahutubia waumini baada ya swala ya Eid iliyoswaliwa msikini hapo, jijini Dar es Salaam.
Sheikh Mapeyo ambaye ni mgombea wa kiti cha Ubunge Jimbo la Kawe kupitia Chama cha Wananchi, CUF, alisema waumini wa Kiislam na wananchi kwa ujumla wasihadaiwe na propaganda za kuchagua viongozi kwa kuangalia chama bali wasifu wa mgombea kwa nia ya kujiletea maendeleo.
Alisema kuendelea kuchagua wagombea kwa kuzingatia chama ndio ambayo yamefanya Tanzania kuendelea kudumaa kwa muda mrefu kwa kuwa wapo baadhi ya wagombea hawana sifa za uongozi lakini wamechaguliwa kupitia vyama vyao.
"Waislam wakati tukizingatia 'darasa' tulilolipata kipindi cha Ramadhani ni vema tukajipanga kwa ajili ya uchaguzi mkuu ujao, tusiupuuze na muhimu ni kuhakikisha tunachagua watu wenye sifa na sio kuangalia chama," alisema.
Aliongeza kwa kuwataka waumini nao na watanzania kwa ujumla kushiriki kwa wingi kwenye uchaguzi huo kwa kujitokeza kupiga kura ili kuhakikisha wanajichagulia viongozi na makini watakaowaletea maendeleo ya maeneo yao.
"Bila kujali jinsia jitokezeni kwa wingi kushiriki kupiga kura Oktoba 31, puuzeni propaganda zinazosambazwa na baadhi ya watu kwamba kushiriki uchaguzi ni haramu, mtajiletea maendeleo vipi kama hampigi kura?" Alihoji.
Sheikh Mapeyo alisema mambo mengi hapa nchini yamekuwa yakienda kombo kwa sababu wananchi wengi wamekuwa sio makini katika kushiriki uchaguzi mkuu ambayo ndio silaha ya kujiletea maendeleo ya kweli.
Uchaguzi Mkuu wa kuchagua madiwani, wabunge na Urais utafanyika Oktoba 31 na kwa sasa wagombea wanaendelea na kampeni zao.
Mwisho
No comments:
Post a Comment