MSHAMBULIAJI nyota wa timu ya Azam, John Bocco 'Adebayor' amesema pamoja na kwamba hajaonyesha makeke yake kwenye msimu huu wa Ligi Kuu Tanzania Bara, bado anatumaini ya kunyakua tuzo ya Mfungaji Bora.
Aidha nyota huyo amekiri kufanya vibaya kwa timu yao katika baadhi ya mechi zake kumewaweka mahali pabaya, lakini anaamini mwisho wa siku wanaoiponda Azam watakuwa wa kwanza kuwapongeza kwa taji la ubingwa.
Akizungumza na Micharazo, Bocco, alisema ingawa amechwa na washambuliaji Jerry Tegete na Mussa Mgosi wenye mabao zaidi yake, bado anaamini ataibuka kinara wa mabao.
Bocco alisema mabao mawili aliyoyapata kupitia mechi mbili ni dalili za wazi kasi yake haijapungua, ila kilichotokea ni hali ya kawaida ya soka lenye ushindani kama ilivyo msimu huu nchini.
"Sina hofu ya kiatu cha dhahabu, kwani najiona nipo vema kutokana na ukweli nimecheza mechi mbili na nina mabao mawili, wakati wenzangu wamecheza mechi kibao wamenipita mabao mawili tu," alisema Bocco.
Kuhusu kuboronga kwa timu yake nyota huyo anayeichezea pia timu ya taifa, alisema ni wameyumba, lakini hiyo haina maana ndoto yao ya kutwaa ubingwa ndio imeyeyuka kwa sababu mechi za ligi hiyo bado zipo nyingi.
"Wanaotucheka sasa ndio watakaokuwa wa kwanza kutupongeza, naamini tutakaa vema na kufanya vizuri katika mechi zetu zijazo kwa vile tuna kikosi kizuri kinachocheza kitimu haswa," alisema Bocco.
Timu hiyo iliyoshika nafasi ya tatu msimu uliopita hivi karibuni iliyumba katika mechi zake tatu baada ya kufungwa na Simba, Kagera Sugara na Toto Afrika kabla ya kuzinduka mwishoni mwa wiki kwa kuilaza African Lyon.
Kikosi cha timu hiyo kimesheheni nyota kama Mrisho Ngassa, Bocco, Kally Ongala, Patrick Mafisango, Peter Ssenyonjo, Jabir Aziz na wengineo.
Mwisho
No comments:
Post a Comment