STRIKA
USILIKOSE
Friday, December 10, 2010
Ally Choki awafunda wanamuziki wenzake
NYOTA wa muziki wa dansi nchini, Ally Choki amewafunda wanamuziki wenzake akiwataka wajenge tabia ya kuwa na shukrani wakikumbuka mazuri wanayofanyiwa na bendi wanazozihama badala ya kuziponda na kutaja mabaya tu.
Choki alisema tabia ya wanamuziki wanaohama bendi kuponda na kukashfu kule watokapo sio tu zinavunja umoja, ila inajenga uhasama miongoni mwa wasanii na wamiliki na mwisho wa siku ni kudidimiza muziki ambao umekuwa ukisaidia vijana wengi kupata ajira zao.
Akizungumza na MICHARAZO, Choki, alisema yeye binafsi pamoja na kutamba kimuziki nchini, katu hawezi kusahau fadhila na mazuri aliyofanyiwa na Asha Baraka, kitu alichotaka hata wasanii wengine wawe na moyo wa namna hiyo wa kukumbuka fadhila.
Choki alisema amelazimika kusema hayo kutokana na baadhi ya wasanii walioihama bendi yake kusambaza maneno ya kashfa juu yake na bendi yake, wakati kabla ya kuhama walikuwa wakifanyiwa fadhila zilizowafanya wamuone kama 'Mungu-Mtu'.
"Siwalazimishi, lakini nawaasa wanamuziki wenzake na wasanii kwa ujumla kuwa na shukrani kwa mazuri wanayofanyiwa na makundi yao, kuhama hakukatazwi, lakini sio kwa kukashfu au kuponda tu, kwani ndiko kunakodumaza muziki," alisema Choki.
Aliongeza kama sio kuwa na moyo wa kutaka muziki wa dansi usonge mbele na kusaidia vijana wengine wenye vipaji kupata riziki kupitia ajira ya sanaa hiyo, asingeanzisha na kuendesha bendi ya Extra Bongo na badala yake angekuwa mwanamuziki wa kujitegemea ili ale kuku kwa raha.
"Kwa jina na umaarufu nilionao ndani na nje ya nchi naweza kuendesha shughuli zangu za muziki kama solo artist, lakini naguswa na kupenda kusaidia wengine kutokana, ili kulifanya jina langu liendelee kutajwa katika mchango wa muziki huu," alisema.
Choki, alisema hata leo Mbaraka Mwinshehe na Marijab Rajab pamoja na kufa wanatajwa kwa sababu waliwasaidia wengi kupitia bendi zao hali ambayo anatamani naye iwe hivyo milele.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment