STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, December 10, 2010

Msondo yamuombea Gurumo



WAKATI hali yake ikizidi kuwa tete, uongozi wa bendi ya Msondo Ngoma umemuombea dua njema na kuwataka Watanzania kuzidi kumuombea kiongozi wao na muimbaji mkongwe wa muziki wa dansi nchini, Maalim Muhidin Gurumo aliyelazwa hospitalini kwa matatizo ya mapafu.
Msemaji wa bendi hiyo, Rajabu Mhamila 'Super D', alisema wanamuziki na uongozi mzima wa Msondo umekuwa ukiendesha dua maalum kila siku kumtakia kila la heri na afueni, Gurumo ili aweze kurejea tena jukwaani.
Super D, alisema Msondo bado inamhitaji mno Gurumo kutokana na umahiri wake katika muziki na uongozi kwa ujumla na kuwaomba mashabiki wao na wadau wa muziki wa ujumla kuzidi kumuombea mwanamuziki huyo mkongwe awe kupona haraka.
"Kwa kweli tunamuombea sana mwenzetu aweze kupona na tunawasihi watanzania bila kujali dini, rangi au kabila na ushabiki wa muziki, wamuombee kamanda Gurumo, Mwenyezi Mungu amfanyie tahafif apone haraka," alisema Super D.
Super D, alisema pamoja na kumuombea kiongozi wao huyo, bendi yao bado inaendelea na maonyesho yao kama kawaida pamoja na kufanya maandalizi ya kufyatua albamu yao mpya.
Alisema kwa leo Jumamosi bendi yao itakuwa kwenye bonanza lao kwenye viwanja vya Sigara, TCC- Changombe na kesho Jumapili watawachezesha wapenzi wa muziki miondoko yao ya Msondo kwenye onyesho litakalofanyika Max Bar, Bungoni Ilala jijini Dar es Salaam.
"Hatuwezi kuacha maonyesho, tunaendelea na shoo huku tukizidi kumuombea mwenzetu, leo (jana) Ijumaa tutakuwa Postal Club, Jumamosi tunaendelea na bonanza letu pale TCC-Chang'ombe na tutamalizia wikiendi yetu kwenye ukumbi wa Maxi Bar, Ilala," alisema.
Msondo inayotamba na albamu ya HUna Shukrani iliyotoka mwaka jana, ipo katika maandalizi ya kutoa albamu mpya ambapo hadi sasa tayari imeshaachia nyimbo tatu ambazo ni Dawa ya Deni, Lipi Jema na Mjomba.

No comments:

Post a Comment