DIWANI wa Kata ya Kimamba, wilayani Kilosa, Amer Lugunga, amefanikiwa kuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya hiyo baada ya kuwaangusha wagombea wenzake wenzake wawili.
Wagombea walioangushwa na Lugunga, ni pamoja na Leonard Mapunda na mtu mwingine aliyetajwa kwa jina moja la Mbiza.
Katika mchuano huo uliofanyika kwenye ofisi za CCM wilaya ya Kilosa, Lugunga aliibuka mshindi kwa kuzoa jumla ya kura 40 kati ya 60 zilizopigwa kwenye kinyang'anyiro hicho kilichokuwa na ushindani mkali.
Mbiza alishika nafasi ya pili kwa kupata kura 17 na Mapunda aliambulia tatu tu.
Akizungumza na MICHARAZO mara baada ya kutangazwa kuwa mshindi, Lugunga alisema atafanya kazi kwa ari zaidi, nguvu zaidi na kasi zaidi kuhakikisha Kilosa inaondokana na aibu iliyoighubika kwa sasa.
"Nawashukuru walionichagua, na ahadi yangu ni kwamba nitafanya kazi kwa ari zaidi, nguvu zaidi na kasi zaidi, ili kuirejeshea heshima wilaya yetu iliyopewa hati chafu hivi karibuni kutokana na matumizi mabaya ya fedha za miradi ya maendeleo," alisema Lugunga.
Alipoulizwa juu ya 'zengwe' alilokuwa akiwekewa na baadhi ya wapinzani wake, Lugunga, alisema mambo yote yameisha na hana kinyongo na mtu.
Mwisho
No comments:
Post a Comment