STRIKA
USILIKOSE
Friday, February 25, 2011
Mabondia kuzipiga kuwachangia wahanga wa mabomu
MABONDIA mbalimbali kutoka mikoa tofauti wanatarajiwa kupigana katika michuano maalum kwa nia ya kusaka fedha za kuwasaidia wahanga wa milipuko ya mabomu ya Gongo la Mboto, jijini Dar es Salaam.
Michuano hiyo itakayochezwa sehemu nne tofauti ndani ya mikoa ya Dar, Pwani na Morogoro, imeratibiwa na kampuni ya Funiko Inc, chini ya uratibu wa mkurugenzi wake, Rowland Raphael Chulu 'Chen Lee Master'.
Chulu alisema michezo ya kwanza itafanyika kwenye ukumbi wa Hugho Tower Pub, Kigogo-Mburahati Machi 6, ambapo yeye atapigana na K kutoka Tanga pamoja na kusindikizwa na mapambano mengine ya utangulizi.
Aliwataja mabondia wengine watakaopigana siku hiyo ni Deus Tengwa atakayepigana na Kitonge wa Arusha, Abbas dhidi ya Abuu, Rahim Cobra na Abdul, Masoud Fighter dhidi ya Mrisho Mwana, Husseni Magali na Idd Rashid na Said Omary atapigana na Jembe wa Majembe.
"Pambano la pili litafanyika Machi 13 eneo la Bunju kwenye ukumbi wa Proud Tanzania, ambapo nitarudiana na K, na wiki inayofuata tutakuwa Bagamoyo kwenye ukumbi wa Police Mass ambapo nitachapana na Juma wa huko huko," alisema.
Alisema onyesho la tatu litachezwa kwenye ukumbi wa Makuti-Pub, Ifakara mkoani Morogoro kwa kuumana na Charles wa huko wakisindikizwa na michezo mingine ya utangulizi.
Chulu, aliyewahi kung'ara kwenye Kick Boxing kabla ya kutumbukia kwenye utayarishaji wa filamu nchini, alisema fedha zote zitakazopatikana kwenye maonyesho ya michezo hiyo zitapelekwa kwa wahanga.
Tangu tukio la milipuko ya mabomu litokee wiki mbili zilizopita watu mbalimbali wamekuwa wakitolea kuwasaidia wahanga, ambapo kesho kwenye uwanja wa Uhuru wasanii wa Bongofleva na wale wa filamu wataumana kusaka fedha za kuwasaoidia wahanga hao wa Gongo la Mboto.
Mwisho
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment