KOCHA wa zamani wa klabu ya Yanga, Kennedy Mwaisabula, ameungana na kocha wa Mtibwa Sugar, Tom Olaba kuilalamikia kadi nyekundu aliyopewa kipa Shaaban Kado, siku chache kabla ya kuvaana na timu ya Simba.
Kado, anayeichezea pia timu ya taifa, Taifa Stars, alionyeshwa kadi hiyo katika mechi baina ya timu yake na Toto Afrika na kumfanya alikose pambano la kesho dhidi yao na Simba litakalochezwa kwenye uwanja wa Uhuru, jijini Dar.
Mwaisabula maarufu kama 'Mzazi' alisema kitendo cha Kado kulikosa pambano la kesho limepunguza ladha kutokana na ukweli kipa huyo ndiye mhimili wa Mtibwa Sugar na hivyo kuipungizia nguvu timu yake.
Kocha huyo aliyewahi kuzinoa timu kadhaa ikiwemo Bandari-Mtwara, Cargo, Twiga Sports, Villa Squad na TMK United, alisema kwa jinsi mazingira ya kadi hiyo ilivyotolewa huko Mwanza anahisi kama kuna 'mchezo mchafu'.
Alisema japo hana hakika, lakini huenda kadi hiyo imetolewa kwa nia ya kuidhofisha Mtibwa katika mechi yao ya kesho, kitu alichodai mambo kama hayo yanachangia kuporomosha kiwango cha soka la Tanzania.
"Nadhani ifikie wakati mambo kama haya ya ujanja ujanja kwa nia ya kuzibeba timu kubwa zikaachwa ili soka lisonge mbele, nimesikitishwa na kadi ya Kado kwa vile imepunguza msisimko kwa pambano lao na Simba," alisema.
Kauli ya Mwaisabula imekuja siku chache, tangu kocha wa Mtibwa, Mkenya Tom Olaba kulalamikia kadi hiyo iliyotolewa na mwamuzi Judith Gamba, akidai imeinyong'onyesha timu yake kwa ajili ya pambano hilo dhidi ya Simba.
Kado alipewa kadi na mwamuzi huyo baada ya kuilalamikia penati iliyopewa wenyeji wao, Toto Afrika ambapo pambano lilishia kwa Mtibwa kushinda 2-1.
No comments:
Post a Comment