STRIKA
USILIKOSE
Wednesday, July 27, 2011
Banka aishtaki Simba kwa TFF
KIUNGO Mohammed Banka ameishtaki klabu yake ya Simba kwa Shirikisho la Soka Tanzania, TFF, juu ya sakata lake la kutaka kupelekwa kucheza kwa mkopo katika timu ya Villa Squad bila ridhaa yake.
Banka, aliyeichezea Simba kwa mafanikio tangu ilipomsajili baada ya kutemwa na Yanga, msimu wa 2008-2009, alisema ameamua kuchukua maamuzi huo kutokana na kuona viongozi wa Simba wanamzungusha kuhusu suala la uhamisho wake.
Mwanasheria aliyepewa kazi ya kumpigania Banka, John Mallya, aliiambia MICHARAZO jana kuwa, wameandika barua Shirikisho la Soka Tanzania, TFF, ili kuingilia kazi suala la mteja wao kabla ya hatua zingine za kisheria kufuata.
Mallya, alisema wameamua kuandika barua hiyo, TFF kutokana na kuona viongozi wa Simba wanakwepa kukutana kulimaliza suala la Banka, kutokana na wenyewe kukiuka mkabata baina yao na mchezaji huyo kama sheria zinavyoelekeza.
Alisema walikuwa katika mazungumzo mazuri na viongozi wa klabu hiyo, lakini juzi walipopanga kukutana ili kulimaliza suala hilo, wenzao walishindwa kutokea na kuona ni vema waombe msaada TFF, kabla ya kuangalia cha kufanya kumsaidia mteja wao.
Afisa Habari wa TFF, Boniface Wambura alikiri kupokewa kwa barua hiyo ya ombi la Banka kutaka shirikisho lao kuingilia kati na kudai itapelekwa kunakohusika kufanyiwa kazi.
"Ni kweli barua hiyo imefika kwetu, Banka akiomba TFF iingilie kati sakata lake la Simba," alisema Wambura.
Naye Afisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga, alikiri kuwepo kwa mazungumzo yaliyokuwa yakiendelea baina ya pande hizo mbili, ingawa alisema alikuwa hajaipata nakala ya barua hiyo ya malalamiko ya Banka iliyopelekwa TFF.
"Hilo la kushtakiwa TFF, silijui kwani sijapata barua, pia siwezi kuliongelea kwa undani kwa vile lilikuwa linashughulikiwa na viongozi wa juu, ambao kwa bahati karibu wote wameenda Uturuki kushughulikia suala la ujenzi wa uwanja," alisema.
Banka, amekuwa akisisitiza kuwa kama Simba haimhitaji ni bora mlipe chake aangalie ustaarabu wake kuliko kumlazimisha kwenda Villa Sqaud iliyorejea ligi kuu msimu huu.
Mwisho
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment