WASANII zaidi ya 100 wa mkoani Morogoro wanatarajia kufanya tamasha kubwa litakaloshirikisha sanaa za aina mbalimbali.
Mratibu wa tamasha hilo lililopewa jina la 'Wakali Concert', Athuman Mswagala 'Mahita' aliiambia Micharazokwa njia ya simu kutoka Morogoro kuwa tamasha hilo litafanyika Julai 30 katika ukumbi wa Vijana Social ulioko mjini hapa.
Mswagala, alisema lengo la tamasha hilo litakalowahusisha wasanii wa mkoa huo wa fani mbalimbali ni kufahamiana na kuibua vipaji vipya.
Alisema maandalizi kwa ajili ya tamasha hilo yanakwenda vizuri na kwamba kinachosubiriwa ni kufanyika kwa tamasha hilo.
Alisema katika tamasha hilo litakalokuwa likifanyika kila mwaka, wasanii watakaofanya vizuri watazawadiwa zawadi mbalimbali ikiwa ni pamoja na fedha taslimu.
"Kimsingi, maandaalizi yanakwenda vizuri na wasanii wengi wamethibitisha kushiriki hali ambayo naamini itakuwa burudani tosha kwa wakazi wa Morogoro" alisema.
Naye, mkurugenzi wa kampuni ya Katundu, wanaodhamini tamasha hilo, Mohamed Katundu, alisema kampuni yake imeamua kudhamini tamasha hilo kwa lengo la kusapoti wasanii wa Morogoro.
Katundu alisema hiyo ni moja ya mipango ya kampuni yake kuhakikisha wasanii mkoani hapa wanapata mafanikio makubwa kupitia sanaa mbalimbali.
No comments:
Post a Comment